CHAMA Cha Mapindunzi (CCM), kimeiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), kufanya uchunguzi kuhusu kujitoa kwa wakandarasi wa miradi ya maji.
Chama kimeshauri kuwa, hatua hiyo ya uchunguzi ni vyema kuanzia katika wizara husika ya maji.
CCM imeahidi kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika, kuona utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan, unafanyika kwa uhakika, lengo likiwa wananchi wapate maji safi na salama.
Akizungumza, alipotembelea mradi huo unaotekelezwa katika Kata ya Bangwe, Halmashauri ya Kigoma Ujiji, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema njia pekee ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji majisafi na salama, mikoa iliyopo karibu na maziwa ni vyema kuhakikisha serikali inakamilisha miradi mikubwa iliyojiwekea.
Alisema ni jukumu la msingi kwa wizara ya Maji hasa ofisi zilizopo katika mikoa yenye ziwa, kuhakikisha wanapunguza au kutatua changamoto zilizopo.
“Wizara ya Maji, hili ni jukumu lenu la msingi, hasa ninyi mliopo ziwani, tunataka tutoke huku sasa, kwa sababu kimbilio pekee la kupunguza au kutatua changamoto ya maji ni kutumia rasilimali ya ziwa.
“Sisi kama Chama, tuna imani kubwa nanyi watendaji mliopewa dhamana ya kusimamia na jitihada hizi mnazofanya, lakini sasa mnahitaji kuongeza umakini na uzalendo, kwani mnaweza kuwa makini, ila uzalendo hakuna, yapo baadhi ya maeneo hadi wakandarasi wanajitoa, kuna mambo mengi nyuma yake,” alisema.
Aidha, alisema katika mradi huo wa maji wa Ziwa Tanganyika, tayari mkandarasi amejitoa kufanya kazi huku akiwa tayari amefanya upembuzi yakinifu na kukubali kufanya kazi.
“Hapa sasa ni mtu mmoja kajitoa, aliyepo hivi sasa ni wa pili. Hii ni shida kubwa ya wakandarasi kuondoka. Jana niliongea na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliniambia anakusudia kukutana na wakandarasi nchi nzima, nadhani hili nalo muhimu.
“Sisi tunawapa kazi, wakandarasi tunawaamini ila sasa wanaturudisha nyuma maana kila siku tunaimba tatizo la maji, ukija huku unakuta mkandarasi kajitoa,” alisema.
Awali, akiwa anawasilisha taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA), Mbike Jones, alisema mradi huo, unatekelezwa na serikali kupitia wizara ya maji.
Alisema wizara imeingia mkataba na mkandarasi Kampuni ya Sino Hydro Corporation kwa ajili ya ujenzi wa kitekeo kipya cha maji katika eneo la Amani beach.
Alisema mradi huo ulisainiwa Novemba 23, 2020 na kuanza kazi Julai 19, mwaka huu ukiwa chini ya wizara hiyo, umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).
Alisema mradi huo unatarajia kukamilika Julai 19, mwakani ambapo shughuli zitazofanyika ni ujenzi wa kituo cha kusukuma maji yasiyosafishwa chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 42,000,000 kwa siku, ujenzi wa bwawa la muda ili kuwezesha ulazaji bomba la kipenyo cha milimita 1,000 la kuchukulia maji ndani ya Ziwa Tanganyika.
Shughuli zingine ni ujenzi wa kambi ya mkandarasi, ujenzi wa barabara ya muda kwa ajili ya kusafirisha vifaa na mitambo ya mkandarasi kufika eneo la kitekeo kipya cha maji na uhamishaji wa pampu za maji yasiyosafishwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda alisema mradi huo umekuwa kitendawili kwa wananchi kwa kuwa umechukua muda mrefu bila ya kukamilika.
Na MWANDISHI WETU, Kigoma



























