KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema CCM inaridhishwa na juhudi za kisera zitokanazo na upeo, uthubutu na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika medani za kimataifa.
Amesema kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia sio ndogo kwani amefanikiwa kuithibitishia dunia msimamo wa taifa, sera za serikali yake kama fahari ya Tanzania na Afrika.
Shaka alieleza hayo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Rais Samia kuwasili nchini alipomaliza ziara yake nchi za Ufaransa na Ubelgiji.
“Rais Samia kila alipopita alikutana na wakuu wa nchi wenzake, pia alikutana na makundi mbalimbali na kutoa hotuba za kizalendo akiweka msisitizo wa mashirikiano ya kikanda na kimataifa na kumfanya ajipambanue kimataifa,” amesema.
Amesema Rais Samia licha ya kuonyesha upeo, maarifa na ufahamu mpana, aliweka bayana msimamo wa nchi yake wenye dhamira ya kudumisha kuendeleza ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
“Rais Samia ni alama mpya ya nchi yetu na kioo cha Afrika kwenye medani za kimataifa. Amekuwa mchapakazi anayesimamia utekelezaji wa sera zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi,” alisema.
Amesema Chama hakikukosea kumfanya kuwa Makamu wa Rais na sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “CCM haina hofu naye hata aliposhika urais baada ya kifo cha Hayati Dk. John Magufuli.”
Amesema kwa jinsi anavyoendelea kuchapakazi amethibitisha ni kiongozi mwenye uwezo na uelewa, huku akimudu vyema kutekeleza majukumu yake na kuonyesha dhamira alionayo.
“Watanzania wamejawa furaha na matumaini kadri wanavyomuona kiongozi wao akihangaika huku na huko. Amefanikiwa kukubalika kimataifa pia akiaminiwa na jumuiya za kimataifa, taasisi za fedha na mashirika ya maendeleo,” amesema.
Aidha, Katibu huyo wa NEC alisema sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania imelenga kuendeleza diplomasia ya uchumi baada ya kupata mafanikio makubwa ya kujitangaza kimataifa, kuelezea sera na misimamo yake tangu awamu ya kwanza hadi ya sita.
Shaka aliongeza kwamba Rais Samia amejenga ukaribu na viongozi wa mataifa yenye uchumi imara duniani na kufanikiwa kukutana na marais wenzake kadhaa kutokana na msingi uliowekwa na watangulizi wake.
“Rais Samia itakumbukwa alianza kuzuru nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki kabla hajatembea mataifa ya Ulaya na Marekani. Amelihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia kukutana na jumuiya za kimataifa,” alieleza.
Aliongeza: ” Kama nilivyosema Rais hatazuiwa kwenda mahali popote. Hatafanya hivyo kwa sababu dunia ya sasa si ile ya rais kujifungia Ikulu. Anapaswa kuingia kwenye mawindo ya diplomasia ya uchumi. Ulimwengu wa leo ni kijiji kimoja kinachotegemeana na wala si muda wa kujitenga.”
Shaka alisema Rais Samia amekuwa akishiriki kwenye meza na majukwaa mbalimbali ya majadiliano ya kisiasa, kibiashara na ya kiuchumi kwa manufaa ya watu na taifa lake.
Alisema kutokana na juhudi hizo amefanikisha kupatikana misaada ya fedha za maendeleo ya kisekta, ambazo zitasukuma mbele sekta za umma ikiwamo kilimo, afya, elimu mazingira, mapambano dhidi ya UVIKO -19 na mabadiliko ya tabianchi.
Na MWANDISHI WETU



























