KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amemtaja Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa turufu ya maendeleo ya Watanzania kutokana na falsafa tatu anazotumia katika uongozi wake, ambazo ni upangaji, usimamiaji na utekelezaji.
Aidha, amemtaja Mkuu huyo wa nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kuwa mwanadiplomasia nguli wa uchumi na hilo linadhihirika kwa namna alivyopata mkopo nafuu kutoka Shirika na Fedha la Kimatafa (IMF) na namna alivyopanga matumizi yake.
Shaka aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akipokea tuzo ya kumpongeza Rais Samia kwa utendaji mzuri, iliyotolewa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema Rais Samia amekuwa turufu ya maendeleo ya watanzania kutokana na falsafa tatu anazozitumia katika uongozi wake ambazo ni upangaji, utekelezaji na usimamiaji.
Kwa mujibu wa Shaka, hayo yamejidhihirisha katika uongozi wake kwa kipindi cha miezi tisa ambapo mambo makubwa yamefanyika.
Alieleza katika kipindi hicho umeshuhudiwa utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025, kwamba wanaamini kufikia mwaka 2025 utekelezaji utazidi asilimia 100.
“Kwa kipindi hiki kifupi cha uongozi wake, leo hii ukimsimamisha Mkuu wa Wilaya yoyote akueleze mafanikio, atatumia zaidi ya saa nane kueleza kazi kubwa iliyofanywa kwa muda mchache,” alisema.
Kwa mujibu wa Shaka, Rais Samia amekuwa kiongozi ambaye kila anachokikusanya anahakikisha kinakwenda katika shughuli lengwa, jambo linalothibitisha usimamizi mzuri.
Aidha, Shaka alimtaja Mkuu huyo wa nchi kuwa mwanadiplomasia nguli wa uchumi kutokana na kile alichoeleza kwamba, amefanikisha upatikanaji wa mkopo nafuu sh. trilioni 1.3 kutoka IMF na ameuelekeza katika matumizi sahihi.

Alisema fedha hizo zimeongeza mzunguko nchini na hivyo kufanya kipato cha kila mtanzania kuongezeka.
Pamoja na mambo mengine, alibainisha tuzo hiyo waliyomkabidhi Rais Samia ni ishara ya vijana kuiunga mkono wa serikali ya awamu ya sita.
Aliwataka vijana kuwa mabalozi wazuri wa Rais Samia kwa kueleza mazuri anayofanya, akiwasihi wasipofanya hivyo hakuna mtu wa nje ya nchi atatekeleza hilo badala yao.
“Mcheza kwao hutunzwa basi nanyi vijana hakikisheni mnakuwa mabalozi wazuri wa Rais wetu, ni sisi ndiyo wa kumtia moyo hakuna mwingine atakayefanya hivyo badala yetu,” alisema.
Aliahidi kuandaa darasa la itikadi kwa ajili ya kuwaelimisha vijana, wafahamu nchi ilipotoka, ilipo sasa na inapoelekea.
Katika hafla hiyo Shaka alipokea wanachama wapya waliojiunga na CCM kutoka UDSM.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la UDSM, Isack Sambuli, alisema tuzo hiyo waliyotoa kwa Rais Samia imetokana na utendaji mzuri aliouonyesha kwa kipindi kifupi.
Aliahidi kumtetea na kumuunga mkono wakati wote, akisema vijana hawatarudi nyuma katika hilo.
Pongezi hizo kwa Rais Samia zinakuja ikiwa ni miezi tisa tangu aapishwe kushika wadhifa huo, huku akifanya mambo makubwa ndani ya muda huo mfupi.
Miongoni mwa mambo hayo ni ushawishi wa upatikanaji wa mikopo nafuu, ukiwemo wa sh. trilioni 1.3 uliowezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 kwa ajili ya shule za sekondari na shikizi nchini.
Pamoja na mikopo, pia Rais Samia kwa kipindi kifupi amekuwa mithili ya nyota inayong’ara kwa kutatua vikwazo vya biashara baina ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Kenya.
Pia, amewezesha kununuliwa kwa ndege mbili zilizofanya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuwa na jumla ya ndege 12, huku nyingine tano zikiwa zimeshaanza kulipiwa.
Kwa kipindi cha miezi tisa amerahisisha mazingira ya biashara na kuongeza idadi ya wanaoonyesha nia ya kuwekeza nchini, huku hali ya siasa ikiwa tulivu kutokana na mikutano yake na wadau wa siasa.
Pia amekuwa akisimamia vilivyo ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, madaraja makubwa na ukarabati wa meli zikiwemo za Ziwa Victoria.
Na JUMA ISSHAKA