KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama hakitaacha kutekeleza malengo yake ya kisera katika kuutumikia umma au kuimarisha uchumi na baadala yake kujielekeza katika kubishana na wapigania vyeo na madaraka.
Shaka aliyasema hayo Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui mjini Unguja, akiwa sehemu ya msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliyeiongoza Sekretarieti katika ziara ya kujitambulisha visiwani Zanzibar.
“Niwasihi wanasiasa nchini wajikite katika siasa za maendeleo kwa kutoa fikra na mawazo mbadala yanayoweza kuchangia kuboresha ustawi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
“Waachane na siasa za kitoto za kutoa mikwara ya maigizo kwa Rais Samia (Rais Samia Suluhu Hassan), wanaompinga wafanye ukosoaji unaojenga na siyo unaobomoa na kutishia kutugawa au kuvunja amani ya nchi,” alisema Shaka.
Shaka alibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha utendaji wa Rais Samia na Rais Hussein Ali Mwinyi, wameakisi mambo yaliyokuwa yakitamaniwa na jamii yatokee na kufuatwa.
Alisema sauti za viongozi hao zimetoa mwanga, kuwapa matumaini mapya waliokata tamaa na tabasamu kutokana na uongozi bora wanaouonesha unaoheshimu taaluma, kusimamia weledi, utawala wa sheria na kutoa uamuzi wa haki.
Alisema CCM Chama kinachounda serikali zinazoongoza nchi, kinapaswa kuwa makini na sikivu kama CCM, hivyo itaendelea kuwa kimbilio la wananchi.
Aliwaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa serikali yao ikiwemo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kusukuma mbele uchumi wa nchi.