SEHEMU YA 2
MTUNZI: CHRISTOPHER LISSA
ISBN ….978-9987-9886-1-7
(Toa maoni ya simulizi hii 0654 58 67 88, 0629 643 419)
ILIPOISHIA……
Naam! Nilipogeuka na kutazama upande wa kile kimsitu cha mikorosho ya Mputa, niliona moto mkubwa ukiwaka juu kabisa ya miti hiyo. Ulikuwa ni moto mkubwa sana.
Hata hivyo nilibaini kwamba moto huo licha ya kuwa mkubwa ulikuwa hauteketezi miti. Ulikuwa ni moto wa miujiza.
Ama kweli dunia hii inamambo na omba uyasikie tu kwa jirani lakini yasikutokee.
SASA ENDELEA……
NURU ilitanda katika eneo lote tulilokuwepo kiasi kwamba nilikuwa mahari peupe kabisa.
Nikabaki nimetumbua macho yangu kwa mshangao mkuu. Mara nikaanza kusikia kicheko cha ajaabu kikitokea katika msitu huo wa mikorosho.
“Haa ..Haaa… Haaaaa…. Haaaaa ,” kicheko chenye sauti mbaya yenye mawimbimawimbi ilipenya sawia katika mifereji ya masikio yangu na kutikisa ngoma za masikio kisha kupeleka taarifa katika ubongo ulioniletea tafsiri ya haraka kuwa kilicho kuwa kikitokea mbele yangu ni tukio la muujiza wa kutisha.
Siyo tukio la kutisha tu, bali muujiza wa kutisha sana. Nikabaki nimeduwaa kama sanamu lililosimikwa katikati ya mbuga hiyo, huku nikiwa nimekodoa macho , akili yangu ikiwa imeruka kwa uoga.
Naam! Sasa ule moto uliokuwa ukiwaka juu ya mikorosho ukajikusanya na kufanya duara moja kubwa.
Taratibu nikaanza kuona taswira za kiumbe wa ajabu ikijiunda katikati ya mduara huo. Baada ya sekunde kadhaa kiumbe huyo wa kutisha akawa amejiumba.
Alikuwa ni mwanamke wa kutisha sana, mwenye kichwa cha fuvu jeusi.
Sura yake ilikuwa ya bibi kizee. Macho yake makubwa ya duara yalikuwa mekundu sana yenye mboni nyeusi kama za paka.
“Haaa! Haaa.. Haaaa,”aliangua kicheko cha kifedhuri. Alikuwa na ulimu mrefu uliokuwa ukiwaka moto mwekundu sana.
Alijifunika mtandio mweupe kuzunguka kichwa chake hadi chini ya kidevu. Sehemu ya chini alivaa nguo pana nyeupe za hariri.
Alikuwa ni mrefu sana lakini mwenye umbo jembamba la duara. Nguo alizo kuwa amevaa zilikuwa zikipepea kutokana na upepo uliokuwa ukivuma.
Hata hivyo kwa chini alikuwa haonekani vema kutokana na kufifia kwake.
Alipokamilika kujiumba, sasa akaanza kupepea angani na kutoka katika mduara wa moto kisha kuja hadi mahari nilipokuwa nimesimama.
Akasimama karibu yangu umbali wa kama hatua tano hivi, huku akiwa anaelea angani.
“Jini?,” akili yangu iliuliza.
“Hapana Shetani!” nafsi ikajibu haraka.
Hata hivyo sikuyatilia uzito majibu yote mawili, kwa sababu akili yangu ilikuwa kama imeganda kabisa. Ilikuwa haifanyi kazi sawasawa kutokana na uoga mkuu kunitawala.
Yule kiumbe akanitazama kwa umakini sana huku akigeuza geuza kichwa chake kama vile ananikaagua.
“Haaa! Haaa Haaaa!,” akaangua kile kicheko chake cha maudhi. Kicheko cha sauti mbaya ambacho kiukweli kila alipokuwa akicheka nilihisi mitetemo ya kuoghofya sana.
“Wewe!” akasema kwa sauti ya mitetemo.
“Unauona.. moto.. ule!?” sasa akaniuliza kwa sauti ya kawaida, huku akinionyesha moto wa ajabu uliokuwa ukiwaka juu mikorosho. Hata hivyo sikumjibu.
“Wewe! Umeuona moto ule?” akaniuliza tena. Awamu hii akaongeza sauti. Lakini sikumjibu. Nikamkazia macho kumtazama usoni.
“Nakuuuliza weweee! Umeona motooooo,?” akaniuliza kwa sauti ya ukali huku akinisogezea shingo yake na kufanya tutazamane uso kwa uso. Awamu hii pia sikumjibu….
“Aaaaaaah! Aaaaaah! Waaaaaah!,” Yule kiumbe akaanza kunizunguka kwa kasi ya ajabu huku akiwa amefura kwa hasira. Akipiga ukulele wa kutisha mno.
Baada ya kunizunguka akajitokeza tena mbele yangu na kuninitazama kwa ghadhabu kuu.
“Aaaaaaaagh….,” akapiga ukulele na kuelea kwa kasi kuelekea katika mduara wa moto. Baada ya kuingia tu katika ule mduara moto ukazimika ghafla.
Giza likawa limetanda katika eneo lote na ule upepo wa ajabu uliokuwa ukivuma ulikoma ghafra. Hali ikarudi kama awali. Hali ya kawaida
***
Katika maisha yangu hili ndiyo lilikuwa tukio la kwanza la ajabu nililoshuhudia. Nilikuwa nikisimuliwa tu lakini sasa nilijionea kwa macho.
Istoshe katika kimsitu hiki cha Mputa sikuwahi kusikia simulizi za kuwepo kwa miujiza ya kutisha kwani shamba hili nililokuwa ninalima lilikuwa lina limwa tangu enzi za babu yangu Lwitiko Lissa, marehemu baba yangu Christopher Mwakitalu na hatimaye mimi.
Hakukuwahi kutokea miujiza kama hii. Nilipagawa na kusimama kwa eneo hilo kama dakika tano hivi akili yangu ikiwa haiko sawa kabisa.
Taratibu fahamu ziliendelea kunirudia. Nikapumua pumzi ndefu na kuishusha taratibu, kisha nikakusanya nguvu na kujiweka sawa.
Hatimaye fahamu zikawa zimenirudia kwa kiasi fulani kwa sababu tangu muujiza ule ulipoanza kunitokea ilikuwa kama nimehama kabisa katika dunia hii.
Baada ya kichwa kukaa sawa kidogo sikuona umumhimu wa kuendelea kulima.
Nikaamua kuanza kuwaswaga makasa wangu kuelekea nyumbani. Kwakweli akili ilikuwa imeivurugika sana.
Wakati ninatembea kutoka shambani kuelekea nyumbani nilianza kusikia sauti za watu wakiongea.
Kwa kuwa barabara ya vumbi ya Kapwili kuelekea Kajunjumele hadi Ziwa Nyasa ilikuwa haiko mbali na shambani kwangu niling’amua kuwa watu hao huenda walikuwa wanaenda kulima au wasafari wanaenda bandarini ziwani.
Kadiri nilivyo kuwa nikisogea karibu na barabara ndivyo sauti zile za watu nilikuwa nikizisikia.
Nilibaini kuwa hawakuwa watu wawili au watatu,bali kundi la watu. Hata hivyo nilipotega masikio ili nijue nini walichokuwa wanazungumza sikuambulia kitu.
Nikiwa nimebakiza kama hatua 15 hivi kufika barabarani, niliona kundi hilo la watu likipita barabarani.
Nilipotazama kwa makini niliona watu hao kama wamebeba maiti aliyeviringishwa katika shuka jeupe kama siyo sanda.
Maiti huyo ndiyo alikuwa akionekana zaidi kutokana na nguo hizo nyeupe zilizomfanya kung’ara gizani.
Ng’ombe wakasima. Nywele zikaanza kunisimka tena. Nilihisi kitu kibaya tena kikienda kutokea mbele yangu.
Nikajibanza nyuma ya ng’ombe na kuchungulia vizuri na kwa umakini mkubwa.
Ingawa kulikuwa giza lakini niliona kama vivuri vya watu. Wakubwa kwa wadogo. Wanawake kwa waume.
Vicheko, vigeregere na sauti za ajabuajabu zilitawala. Lugha waliyokuwa wakiitumia sikuilewa. Pia japo walikuwa wakitembea lakini walikuwa kama wanaelea hewani.
“Wachawi,” hisia zangu zikaniletea jibu.
“Wafu!” akili na hisia vikaanza kubishana tena.
“Majini?,” ubongo ukauliza swali.
“Au mashetani?” sasa vyote yaani, akili, hisia, ubongo vikauliza swali kwa jumla. Hivyo nikaona vyote havina msaada wa kunipa jibu sahihi. Nikavipuuzia.
Nikaachana navyo nikaona nivema kuhamia moyoni. Huenda moyo ukanipa msaada kwa wakati huo.
Moyo ukanipa ujasiri. Naam! Sasa nikapata mtetezi wangu haswaa. Ujasiri, kwani tukio hili la pili pia nilikwisha baini ni la kutisha kama lile la mwanzo.
“Hili tena?” nikajiuliuza… USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA 3 YA RIWAYA HII YA KUSISIMUA KESHO