SEHEMU YA 3
ILIPOISHIA…
Moyo ukanipa ujasiri. Naam! Sasa nikapata mtetezi wangu haswaa. Ujasiri, kwani tukio hili la pili pia nilikwisha baini ni la kutisha kama lile la mwanzo.
“Hili tena?” nikajiuliuza.
MTUNZI: CHRISTOPHER LISSA
ISBN ….978-9987-9886-1-7
(Toa maoni ya simulizi hii 0654 58 67 88, 0629 643 419)
SASA ENDELEA…
SIKUELEWA ni kwanini yananitokea haya kwa wakati mmoja. Sikuelewa kabisa. Kwakweli nilikuwa katika wakati mgumu mno.
Baada ya lile kundi dogo la watu kupita nikaanza kuwaswaga ng’ombe wangu. Tukakatisha katika ile barabara. Nikashika kinjia kidogo kilichoelekea nyumbani.
Wakati nilipovuka tu mara nywele na mwili wote ukanisisimka. Nilihisi kitu nyuma yangu .
Nilipogeuka ghafla nikaona mtu akinifuata huku akiongea lugha isiyo eleweka. Nilihisi anaongea na mimi.
“Tuko wote?” nikamuuliza kwa pupa, huku nikijitahidi kuficha sauti ya uoga niliyokuwa nayo.
Aliposikia hivyo, akasimama ghafla na kusonya.
“Mfyuuuuu” kisha akageuka nyuma na kutoweka ghafla kimiujiza.
“Duh!” niliguna, baada ya kubaini hakuwa mtu wa kawaida. Nilihisi alikuwa miongoni mwa lile kundi la wachawi lakini alipotea njia na kuanza kunifuataakihisi namimi ni mmoja wao.
Wakati naendelea kutembea ndipo hisia zilizpo nijia kwamba jirani na eneo hilo kulikuwa na Bwawa linalofahamika kama Kyupila.
Niliwahi kusikia katika bonde hili wachawi wanalitumia kula nyama za watu. Hivyo basi nilivuta tena hisia kuwa huenda kundi hilo lilikuwa ni la wachawi na walikuwa wamebeba mtu ambaye walikuwa wakienda kula katika lile Bonde la Kyupila
Kwa mwendo niliotumia kurudi nyumbani tayari kulikuwa kumeanza kupambazuka.
Nilikuta mke wangu Petty amekwisha amka na yuko nje ya nyumba akiwaandaa watoto wangu Neema mwenye umri wa miaka 12 aliyekuwa anasoma darasa la tatu na Eria mwenye umri wa miaka tisa aliyekuwa anasoma darasa la pili.
Wote walikuwa wanasoma katika Shule ya Msingi Kapwili ambayo pia mimi nilihitimu elimu yangu kabla ya kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza na cha nne katika Shule ya Sekondari ya Itope.
“Shikamoo baba,” watoto wangu walinisabahi.
“Marahabaa! Hamjambo?”
“Hatujambo baba. Pole kwa kazi,”
“Ahsante!” nilijibu huku nikiingia ndani.
Baada ya watoto kuelekea shuleni, mke wangu akaja ndani.
“Vipi Baba Neema? Mbona mapema leo kwema huko kweli?”
“Huko kwema tu,” nilimjibu.
“Mh! Lakini mbona unaonekana mnyonge?” mke wangu alizidi kunidadisi.
“Kwema tu mke wangu. Jembe limeharibika ghafla,” nilimdanganya mke wangu, huku nikijitahidi kutokuonyesha hofu niliyo kuwa nayo kutokana na mambo yaliyokuwa yamenitokea.
“Duh! Pole sana. Ndiyomaana nimeshangaa kuona umerudi mapema leo. Najua we muda wako wa shambani kurejea hapa saa tatu au saa nne. Kumbe umeharibikiwa? Pole,”alisema mke wangu ambaye kwa kweli alikuwa ni faraja kubwa kwangu.
Nilimpenda na yeye alinipenda kwa dhati. Kifupi tulipendandana. Lakini sikutaka kuumsimulia chochote.
Tangu enzi za mababu tuliambiwa kuwa ukikutana na jambo la ajabu usihadithie kwa mtu yoyote siku hiyo hiyo au muda mfupi baada ya kuona la sivyo litakuathiri zaidi ama utakufa.
Hii imani ilitupa ujasiri wa kuhifadhi mambo moyoni kisha kuyahadithia baada ya kitambo fulani. Hali hiyo ilisaidia jamii pia kutoishi kwa woga.
Mchana ulipita. Jioni ikaingia hatimaye ukawa usiku. Kiukweli mchana wa siku hiyo ulikuwa ni mrefu sana kwangu.
Licha ya kuilazimisha furaha, lakini ndani ya moyo wangu nilikosa amani kabisa.
Yale matukio yalikuwa yakijirudia akilini mwangu kama sinema ya kutisha na kuogofya sana.
Ile taswira ya yule kiumbe wa kutisha bado nilikuwa kama naiona dhahiri mbele yangu.
Kicheko cha ajabu kilikuwa kikisikika kikivuma akilini mwangu na kunifanya mara kwa mara kushituka.
“Oh! Mungu wangu! Nini hiki?” nilijisema nikiwa nimejipumzisha sebuleni katika nyumba yangu yenye vyumba viwili iyojengwa kwa udongo lakini ikiwa imeezekwa kwa bati. Tayari tulikuwa tumekwisha kula.
Ilikuwa ya pata kama saa 3:30 hivi usiku. Watoto walikuwa tayari wamelala.
Mke wangu pia alikuwa amekwisha ingia chumbani kwaajili ya kwenda kuandaa kitanda kisha kulala.
Nikiwa nimekaa katika sofa langu kuukuu la kizamani sebuleni. Usingizi mzito ukaanza kuninyemelea. Hata hivyo nilijihisi uvivu sana kunyanyuka na kwenda chumbani kulala.
Mwili ulikuwa mzito kuinuka. Nikajikuta nikiwa nimeganda katika sofa hilo huku nikisinzia. Hatimaye usingizi mzito ukanichukua.
Nikiwa usingizini ghafla nikachukuliwa kama kwenye maono. Niliona paa la nyumba yangu likifunguka.
Angani nikaanza kuona ule mduara wa moto wa yule kiumbe wa kutisha aliyekuwa amenitokea alfajiri kule shambani ukishuka taratibu. Ulishuka hadi ndani nilipokuwa nimekaa pale sebureni.
“Chriss,”sauti tamu na nyororo iliniita. Nikajihisi kama ninafumbua macho na kutazama mbele yangu.
Niliona ule mduara wa moto wa yule kiumbe. Hata hivyo awamu hii niliona mambo ya tofauti sana…
USIKOSE KUFUATILIA SEHEMU YA 3 YA RIWAYA HII YA KUSISIMUA KESHO