“MIMI napendelea muhogo wa kuchemsha au wa kukaanga ingawa mara nyingine ninasukumia kwa chapati, maandazi au vitumbua,”
Ni kauli ya mkazi wa Kihonda mjini Morogoro, Pendo William, ambaye ni mjamzito anayetarajia kujifungua mtoto wa tatu, endapo mambo yatakwenda vizuri katika safari yake miezi tisa.
Anataja vyakula hivyo baada ya kuulizwa na mwandishi makala hii kuhusu chakula anachokula kila siku kwa ajili yake na mtoto aliyeko tumboni.
Pendo anasema kwa kawaida asubuhi hunywa chai ya rangi na muhogo, mchana ugali wa sembe kwa nyama au samaki, ingawa anasema wakati mwingine samaki humpa hali ya kichefuchefu.
“Niliwahi kuambiwa kwam¬ba kwa hali yangu (ya ujauzito) kula samaki ni muhimu, kwa hiyo huwa najilazimisha kula, ili kujenga afya,” anasema.
Kuhusu mlo wake wa usiku Pendo anaeleza kwamba mara nyingi ni wali kwa maha¬rage, au samaki na kwamba mara moja moja akiwa na fedha ananunua chipsi kwa kuku ‘kushushia’ na soda baridi.
Kuhusu mboga za majani na matunda katika mlo wake, anasema anatumjia lakini sio kitu anachozingatia sana
“Kuna wakati nikiwa na hamu ya mlenda, kisamvu au tembele ndio ninanunua. Mimi napenda kisamvu na mlenda hivyo angalau kwa wiki ninakula moja wapo,” anasema Pendo.
Hata hivyo Pendo anasema si mpenzi wa matunda, lakini anasema huwa anakula mara moja pale mume wake anaponunua, lakini yeye si rahisi kutoa fedha yake kununua tunda.
Nilimuuliza Pendo kama anajua lishe ni nini? Majibu yalikuwa kama ifuatavyo:- Ninachofahamu lishe ni ule unga maalumu uliochanganywa na mahindi, mtama , soya na ulezi
Msingi wa swali ilikuwa ni kutambua ni kwa namna gani anafahamu kuhusu lishe na umuhimu wake kwa siku 1000 za mtoto, lakini ukweli bado kuna changamoto katika jamii.
Pendo anawakilisha wazazi wengi wakiwemo kina baba, ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu siku 1000 za makuzi ya mtoto, kuanzia mimba inapotungwa.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu wa Panita, ambayo ni taasisi inashughulika na lishe, Jane Msagati, siku 1,000 huhesabiwa toka mimba inapotungwa mpaka mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili.
Jane anasema siku hizo ni muhimu, kwa kuwa ndio msingi wa maisha ya binadamu yeyote.
Anasema wazazi ni muhimu kuzingatia lishe bora katika siku hizo1,000 kwa kuwa matokeo yake huendelea kwa kipindi chote cha maisha ya mwanadamu na kwamba mtoto akisha athirika katika siku hizo, kutokana na upungufu wa lishe huwezi tena kurekebisha upungufu huo.
Umuhimu wa siku 1000, Jane anasema lishe bora kwa siku hizo huokoa vifo vya watoto zaidi ya 1,000,000 kwa mwaka duniani, hivyo kama zitatumika vizuri huongeza kiwango cha uelewa wa mtoto na kumwezesha kufanya vizuri shuleni na maishani kwa ujumla.
Hii inatokana na ukweli kwamba mtoto akikosa lishe bora katika hizo siku 1,000, mara nyingi hupata udumavu ambao ni hali ya ubongo na mwili wake, kutokuwa katika kiwango kinachotakiwa.
Kiuchumi, kwa mujibu wa Jane, siku hizo 1,000 kama mama atakula lishe bora wakati wote na mtoto, huongeza uchumi wa nchi kwa maana ya kumwezesha mtoto huyo akikuwa kuzalisha pato la mwaka la (GDP) kwa asilimia 2-3.
“Siku hizi zikizingatiwa na wazazi kwa maana ya lishe bora kwa mama na mtoto, akishaza¬liwa hadi kuadhimisha miaka miwili ya kuzaliwa, hupunguza uwezekano wa magonjwa ya muda mrefus) na mzio,”anasema Jane.
LISHE BORA
Mratibu huyo anafafanua kwamba, lishe ni hali ya mwili kupokea chakula chenye virutubisho vyote muhimu, ambavyo hujenga, kuukinga na kuupa joto, hivyo kuuwezesha kufanya kazi vizuri.
Anataja virutubisho hivyo kuwa ni protini, wanga, vitamini, madini, nyuzi nyuzi na maji.
Anasema matatizo makuu ya lishe nchini, yamegawanyika katika makundi matatu.
Upungufu au tapiamlo wa protini na wanga, upungufu au utapiamlo wa virutubisho vya vitamini na madini na hivi karibuni kumekuwa na utapiamlo utokanao na unene kupita kiasi.
“Lakini upungufu wa virutubisho vya vitamini na madini ndiyo unaoathiri zaidi, sehemu kubwa ya jamii na waathirika wakubwa ni watoto walio katika umri wa chini ya miaka mitano na wanawake walio katika umri wa uzazi,”anasema.
Jane anafafanua kwamba kwa kuwa mwili wa binadamu hauna uwezo wa kutengeneteza virutubisho, chanzo kikuu chake ni kutoka kwenye chakula. Inatakiwa mtu, hususani mtoto na mama mjamzito, kula vyakula vinavyohitajiwa na mwili kila siku na siyo kile kina chomfurahisha tu.
Mtaalamu huyo wa lishe anataja vyakula hivyo, ni wanga kama ugali wa unga usiokobolewa, wali na maandazi), protini (nyama, maziwa, mayai na maharage), vitamini na madini, vitu ambavyo vinapatikana zaidi kwenye matunda na mbogamboga.
Kwa mantiki hiyo, utaona kuwa Pendo ambaye ni mjamzito, hapati lishe inayotakiwa. Anapata wanga na protini lakini hali vya kutosha mbogamboga na matunda, vyakula ambavyo vitamsaidia kumuongezea vitamini na madini mbalimbali.
Lakini mbaya zaidi, anakula ugali wa sembe, ambao ni sawa na kula makapi, anakula chipsi na mayai au kuku wa kisasa, ambao pia watalaamu wanasema ni chakula kisicho na virutubisho muhimu kwa binadamu.
Mambo muhimu siku 1000.
Jambo kubwa kuzingatia ni lishe bora ya mama mjamzito kama Pendo katika kipindi chote cha ujauzito na kufuatiwa na lishe bora ya mtoto tangu anapozaliwa hadi atakapofikisha umri wa miaka miwili na kuendelea.
Kadhalika, Jane anasema mtoto anatakiwa anyonye maziwa ya mama to kwa miezi sita ya kwanza.
“Baada ya miezi sita, mtoto alishwe vyakula vya ziada vyenye virutubisho vyote, wakati huo huo aendelee kunyonya maziwa ya mama yake,” anasena Jane.
Anaongeza kwamba hii ya kunyonyesha mtoto inamfanya pia mtoto kuwa karibu zaidi na mama yake.
Jane anasema ni muhimu mama anayenyonyesha ahakiki-she anapokwenda kwa daktari kama anaumwa amwambie mara moja, bila kusubiri kuulizwa kuwa ananyonyesha ili asije akapewa dawa itakayokwenda hadi kwenye maziwa.
Anasema dawa kama hizo mbali na kumdhuru mtoto husababisha mtoto kukataa kunyonya kabisa, baada ya kusikia harufu au ladha ambayo hakuzoea.
“Unajua mtoto anasikia sana harufu na ladha. Ndio maana mjamzito anatakiwa kuangalia anapoumwa kama dawa anayotaka kunywa inafaa kwa mama mjamzito au la.
Kingine cha muhimu, mama anay¬enyonyesha hatakiwi kunywa pombe, kwa sababu harufu yake ina kawaida pia ya kukimbilia kwenye maziwa. Hiyo inaweza kumfanya mtoto akatae kunyonya,” anasema Jane.
Anasema lingine la muhimu ni kuhakikisha kwamba mtoto anapata chanjo zote zilizoidhinishwa na serikali, pia ku-nakuwa na matumizi ya kutosha ya chumvi yenye madini joto.
Lingine analosisitiza Jane ni familia kumpa mama msaada wa kutosha kipindi chote cha kuanzia ujauzito, hadi kulea mtoto, ikiwamo baba kuwa naye karibu, kula naye na kumsaidia shughuli.
“Mama anapokuwa katika miezi mitatu ya kwanza baada ya kushika mimba, yaani wakati mwili unapokuwa ukipambana kwa kudhani kuna kitu kibaya kimeingia mwilini, yaani ule wakati wa kutapika mara kwa mara, baba anatakiwa kuwa karibu na mkewe hasa kipindi cha kula, ili kumhimiza kula.
“Kama nilivyosema, muda wote wa ujauzito mama anapaswa kula lishe bora na inapendeza zaidi, hata kabla ya kushika mimba mama ajiandae kwa lishe bora kwanza,”anasema Jane.
Mtaalamu huyo wa lishe anasema ni muhimu baba ahusike kipindi chote cha mimba na ulezi wa mtoto ikiwemo kwenda kliniki, kuhakikisha kuna chakula cha kutosha, kutibu magonjwa yanayojitokeza na kumtia mama moyo wakati wote wa malezi ya mimba na mtoto.
Lingine la kuzingatia, anasema ni kuhakikisha vyakula vinaandaliwa katika mazingira safi na salama.
“Lingine ambalo wengi tunapuuzia ni kuboresha hali ya chakula katika kaya. Hili linaweza kufanywa kwa kutengeneza bustani ndogo kuzunguka nyumba au kama hakuna nafasi unaweza kufanya bustani ya makasha au viroba” anasema Jane.
Jane anashauri pia familia kufuga wanyama wadogo wadogo, kama kuku, sungura na kukausha mboga mboga wakati wa masika na kuhifadhi kwa ajili ya kiangazi.
“Ni muihimu katika lishe ya mama na mtoto kuongeza vitu vya asili kama karanga kwenye mboga ili kuongeza virutubishi. Kadhalika tumia vizuri vyakula vinavyopatikana kirahisi katika mazingira yako ili kupunguza gharama, lakini la msingi ni kuhakikisha vyakula ya lishe,” anasema Jane.
Minza Mathias mkazi wa Kihonda Morogoro , anasema wanawake wengi hawana uelewa mzuri juu ya lishe bora, lakini pia kuwa na maisha duni, kunachangia wajawazito kukosa lishe bora, jambo ambalo limekuwa likichangia tatizo udumavu nchini.
Na MWANDISHI WETU