WAKATI Kagera Sugar ikipania kurudi na pointi tatu nyumbani, Kocha wa Simba, Pablo Franco, amesema kikosi chake hakitopoteza mchezo dhidi ya wakata mua hao.
Leo saa moja usiku, Simba itaikaribisha Kagera Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Wekundu wa Msimbazi wataingia katika mchezo huo na matumaini ya kupunguza idadi ya pointi dhidi ya Yanga, katika vita ya kuwania ubingwa msimu huu.
Simba itaingia na matumaini hayo, baada ya mahasimu wao Yanga, kupata suluhu ilipocheza na Prisons, juzi.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba iliyokuwa ugenini, ilikubali kichapo cha bao 1-0, lilofungwa na Hamis Kiiza, katika Uwanja wa Kaitaba mjini Kagera.
Kocha wa Simba, Pablo, alisema mchezo huo unaweza kuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao ila hawatakubali kupoteza.
Pablo, alisema Kagera ina kikosi chenye uwezo na anakumbukumbu za kichapo ilichopokea katika mechi ya raundi ya kwanza.
“Mchezo utakuwa mgumu, Kagera ni timu nzuri na tunakumbuka walitufunga katika mzunguko wa kwanza, lakini hatutakubali kuona tunapoteza mchezo huu, ni muhimu kuondoka na alama tatu,” alisema.
Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Buberwa Bilikesi, alisema timu imeandaliwa vizuri na wachezaji wapo tayari kwa mchezo.
“Tumejipanga vizuri, tupo ugenini lakini hatutakubali kupoteza, tunataka kurudi na pointi tatu muhimu,” alisema.
Katika msimamo wa ligi, Simba iliyocheza michezo 22, inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 46, chini ya Yanga inayoongoza msimamo kwa alama 57, katika michezo 23.
Simba inahitaji ushindi katika mchezo wa leo, ili kupunguza idadi ya pointi dhidi ya Yanga, iwapo itashinda, itabakiza pengo la alama nane.
Kagera Sugar ipo katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 29, inahitaji ushindi ili kukwea hadi katika nafasi ya nne, inayoshikiliwa na Geita Gold, yenye pointi 31 katika michezo 22.
Na NASRA KITANA