WAKATI ikipangwa katika kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), benchi la ufundi la timu ya Simba, limesema litatumia vyema mechi zake za nyumbani ili kupenya katika robo fainali ya michuano hiyo.
Jana mchana, wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu, wamepangwa katika kundi D na timu za RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast) na USGN ya Niger.
Katika michuano hiyo, Simba itaanza kuvaana na Asec Mimosas katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Februari 13, mwakani kabla ya kucheza na RS Berkane anayoitumikia mchezaji wake wa zamani, Mzambia Clatous Chama na aliyekuwa winga wa Yanga, Tuisila Kisinda.
Akizungumzia kundi hilo, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Suleimani Matola, alisema watahakikisha wanajipanga vizuri ili kutinga hatua inayofuata.
Alisema kila timu ina malengo ya kupenya hatua ijayo, hivyo watahakikisha wanafanya maandalizi ya mapema ili kupata pointi tatu katika kila mechi.
“Kila timu tuliopangwa nayo ipo vizuri, sisi kama makocha tutahakikisha tunafanya maandalizi ya mapema na kuwajenga wachezaji wetu ili tuweze kushinda hasa katika michezo tutakayocheza nyumbani, hatutokubali kupoteza pointi tatu,” alisema.
Naye kiungo wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay, alisema kikosi hicho kitakiwa kujipanga vizuri ili kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani.
Alisema katika kundi hilo, timu tishio zaidi ni RS Berkane, anaamini kama Simba itajipanga vyema ina nafasi ya kupenya katika hatua ya robo fainali.
“Kikubwa ambacho Simba itaweza kufanikiwa ni kuhakikisha wanatumia vizuri uwanja wake wa nyumbani, kwani wakifanya hivyo wana asilimia kubwa ya kutinga robo fainali,” alisema Mayai.
Licha ya kundi la Simba, timu za Pyramids ya Misri, CS Sfaxien (Tunisia), Al Ahly Tripoli (Libya) na Zanaco ya Zambia zimepangwa kundi A wakati kundi B likiwa na timu za TP Mazembe (DRC), AS Otohi (Congo-Brazzaville), Cotton Sport (Cameroon) na Al Masry ya Misri.
Kundi C la michuano hiyo lina timu za JS Saoura ya Algeria, Al Ittihad ya Libya, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na mshindi wa jumla kati ya JS Kabylie ya Algeria na Royal Leopard ya Eswatini.
Royal Leopard iliilaza JS Kabylie 1-0 katika mechi ya kwanza nyumbanii, kabla ya mechi ya marudiano kusogezwa mbele hadi Januari kwa sababu ya UVIKO-19.
Na NASRA KITANA