KLABU ya Simba, imeingia mkataba wa miaka miwili na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), kuisafirisha timu hiyo kwa safari zake za ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuingia makubaliano hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amesema mkataba huo unathamani ya zaidi ya sh. milioni 400.
Amesema walianza mazungumzo na kampuni hiyo tangu Aprili mwaka huu, pia wanawashukuru kwa mkataba huo ambao wanaamini unaongezea kuifanya Simba iwe kubwa.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, amesema wameamua kuingia mkataba na Simba kwa kuwa ni klabu kubwa na wanaamini itawatangaza katika mataifa mbalimbali.
“Kwa mfano kama timu ya Simba Queens kwa msimu ujao itakuwa inavaa jezi yenye nembo ya Air Tanzania, kwa kufanya hivi naamini tutakuwa na wateja wengi zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa, mashabiki wa Simba ambao wanataka kusafiri na timu yao, wanaweza kuanza kutoa kidogo kidogo hadi watakapomaliza na kupatiwa tiketi ya safari yake anayotaka kwenda.
Na ELIZABETH JOHN