MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara timu ya Simba, jana wamezindua slogani yao ya “its not over, kazi iendelee”, ambayo wamepanga kuingia nayo Jumapili katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Simba ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 10;00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, watashuka dimbani wakiwa na mtaji wa mabao 2-0 ambao waliyapata ugenini, Oktoba 17 jijini Gaborone, Botswana.
Timu hiyo inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare na kama kufungwa isizidi bao moja, ili kujihakikishia tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya klabu barani Afrika.
Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ally Shatry, alisema baada ya timu hiyo kushinda ugenini anaamini kazi haijaisha, hivyo wanatakiwa kuendelea kupambana ndio maana ya ‘slogan’ hiyo waliyoizindua jana.
“Tulishinda ugenini, tunakuja kupambana hapa nyumbani tunaamini wachezaji wetu wanatambua umuhimu wa kushinda mchezo huu hapa nyumbani,” alisema.
Shatry alisema kwa asilimia 80
wamefanikiwa kufanya maandalizi ya mchezo huo ambao wanaamini utakuwa mgumu kwa kuwa wanahitaji kutinga hatua ya makundi ili kuendelea mbele katika michuano hiyo.
Alisema wapinzani wao walitua Dar es Salam juzi kimya kimya, hata hivyo ametamba wajiandae kupokea kipigo cha pili hapa nchini.
“Tulikaribishwa vizuri tukiwa Botswana na hakukuwa na kitendo chochote kibaya ambacho ni hujuma, tunawakaribisha sana wapinzani wetu wajisikie wapo nyumbani lakini kipigo kipo pale pale,” alitamba.
Alisema wachezaji wao wapo fiti na wameanza mazoezi isipokuwa, mshambuliaji Chris Mugalu na kiungo Pape Sakho ambao wanaendelea kuuguza majeraha.
VIINGILIO VYATAJWA
Viingilio katika mchezo huo ambao utakuwa na watazamaji 15,000, vimetangazwa kuwa sh. 5,000 kwa viti vya mzunguko, sh. 20,000 VIP B, C sh. 40,000 na VIP A sh. 150,000 kwa wateja wa Platinumz.
Na ELIZABETH JOHN