Na NASRA KITANA
SIMBA leo inatarajia kuikaribisha Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kila moja ikitaka pointi tatu muhimu, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi.
Simba inahitaji pointi tatu katika mchezo wa leo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, huku Mbeya City ikihitaji pia alama tatu ili kujinasua katika janga ya kushuka daraja.
Timu hizo zilipokutaka katika mchezo wa kwanza, ambapo Mbeya City walikubali kichapo cha bao 1-0 mchezo, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mjini Mbeya, bao pekee lilifungwa na John Bocco.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleimani Matola amesema wamejipanga kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara nyingine msimu huu.
Matola amesema wanahitaji pointi sita ili kuweza kutangaza ubingwa mapema, hivyo hawatakubali kupoteza mchezo huo kwani utawasogeza mbele katika malengo yao.
Amesema anajua mchezo hautakuwa rahisi sababu Mbeya City nao wanahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kuendelea kubakia katika ligi msimu ujao.
“Najua mchezo hautakuwa rahisi kwetu kwani Mbeya City nao wanahitaji ushindi ili waweze kujihakikishia nafasi ya kuendelea kubakia katika Ligi Kuu msimu ujao, tumejipanga vyema na hatuna mpango wa kupoteza,” amesema Matola.
Naye Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Mathias Wandiba, amesema wamekuja kuchukua pointi tatu muhimu katika mchezo huo.
Amesema wanatambua Simba ina wachezaji wazuri na wenye kiwango bora, lakini wasitegemee kupata mteremko katika mchezo huo.
“Tumekuja tukiwa kamili wachezaji wote wapo fiti, na hakuna anayetaka kupoteza katika mchezo unaofuata, kila mmoja anatambua umuhimu wake na kwamba Simba wasitarajie mteremko,” amesema.
Nahodha wa Mbeya City, Mpoki Mwakinyuke, alisema timu yao ipo vizuri na wamekuja kupambana kwani hawaiogopi Simba ila wanaiheshimu kama zilivyo timu zingine.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba ipo kileleni ikiwa na pointi 70 wakishuka dimbani mara 28, Mbeya City wao wakiwa nafasi ya 13 kwa pointi 36 na kushuka dimbani mara 31.