UTANGULIZI
KATIKA kuongeza Burudani kwenu wasomaji wetu, tumeamua kuwaletea Simulizi za kusisimua ambazo zitakuijia kila Jumatatu hadi Ijumaa, kwa kuanzia anza kufuatilia SIMULIZI YA SIKU YANGU YA KWANZA KABURINI
MTUNZI: CHRISTOPHER LISSA
ISBN ….978-9987-9886-1-7
(Toa maoni ya simulizi hii 0654 58 67 88, 0629 643 419)
ULIKUWA ni usiku wa manane. Giza totoro lilifunika sura ya Dunia. Sauti za wadudu, ndege na wanyama hususan mbwa, paka na komba zilikuwa zikisikika mara kwa mara.
Hii ilikuwa ni kawaida hasa kwa eneo hili la Kijiji cha Kandete, Kata ya Kajunjumele, Wilayani Kyela, mkoani Mbeya.
Kijiji ambacho kiko kilomita 10 tu kutoka Halmashauri ya Mji wa Kyela, unaosifika kwa kilimo cha mpunga, korosho na kokoa pamoja na shughuli za uvuvi hasa katika Ziwa Nyasa, mito na mabwawa.
Nililijinyanyua kiuvivu uvivu na kukaa kitako katika ukingo wa kitanda.
Nikafikicha macho ili kuweka mboni zangu sawa na kupata upeo bora zaidi kutokana na kiza kilicho kuwa kimetanda chumbani.
Mke wangu Petty alikuwa bado usingizini. Sikutaka kumwamsha. Nikamuacha aendelee kulala.
Nikajinyanyua na kupapasa kwa mkono wangu wa kulia katika kimeza kidogo kilichokuwa chumbani humo.
Nikapata kibiriti, ambapo nikachomoa njiti moja na kuiwasha, kisha nikakoleza utambi wa kibatari kilicho kuwa katika kimeza hicho.Mwanga ukatanda chumbani humo.
Nikatazama saa kupitia kisimu changu cha mkononi, ilikuwa ikionyesha ni saa 10:45 usiku.
Naam! Ulikuwa ni muda muafaka kuamka, tayari kwa kwenda shambani kwaajili ya kulima.
Ulikuwa ni msimu wa kilimo kwaajili ya kupanda mpunga, hivyo kwa ukanda huu wa Wilaya ya Kyela, ni kawaida watu kuamka kwenda kulima kuanzia saa 9 usiku.
“Sijachelewa sana…,” nilijisemea huku nikivaa mavazi yangu rasmi kwaajili ya shughuli za kilimo.
Pia nikachukua sime na kulifutika katika mshipi wa suluali yangu kiunoni kwaajili ya usalama.
Baada ya kujiweka tayari sasa nikamuamsha mke wangu ili kumuaga.
“Mama Neema… Mama Neema…” nilimwita huku nikimpapasa.
“Mhhhh!,” aliitika kivivu kutoka katika lindi la usingizini. Akafumbua macho taratibu na kunitazama kabla haja kaa kitako kitandani.
“Mimi naelekea shambani… njoo ufunge mlango,” nilimweleza.
“Haya mume wangu… kila lakheri,”aliniambia huku akishuka kitandani na kuanza kunifuata hadi sebuleni ili afunge mlango.
Nilipotoka nje tu mke wangu akatumia fursa hiyo kuwawekea maji watoto kujisaidia.
Mimi nikalekea katika zizi la ng’ombe kwaajili ya kuwandaa maksai ninao watumia kulima.
Walikuwa ni ng’ombe madume wawili ambao kiukweli nilikuwa nawapenda sana kwa sababu walikuwa wakinisaidia mno katika shughuli za kilimo kuanzia kulima mashamba na kusomba mazao wakati wa mavuno.
Baada ya kuwandaa safari ya kuelekea shambani ikaanza. Shamba lilikuwa umbali wa kilomita tatu hivi kutoka nyumbani kwangu.
Lilikuwa katikati ya mbuga kubwa isiyo na miti wala vichaka, zaidi ya kimsitu kidogo kilicho kuwa kinafahamika kama Kwa Mputa.
Shamba langu lilikuwa hatua chache tu kutoka katika kimsitu hicho cha mikorosho ambacho wakati wa mchana tulitumia kujipumzisha kutokana na kuwa na kivuri safi cha mikorosho.
Mwendo kama wa saa moja hivi, hatimaye nilifika shambani na kazi ya kulima ikaanza.
“Kwenda!! Kwenda!..,” nilimaka huku nikiwa swaga maksai wangu kwa fimbo ndefu.
Mkono mmoja nilitumia kushika mpini wa jembe aina ya plau lililokuwa likikokotwa na maksai hao.
Maksai hawa walikwisha pewa mafunzo maalumu ya kulima hivyo hawakuwa na shida sana. Tukaendelea kulima.
Haiukupita nususaa, mara nikaanza kuhisi kiupepo kilichoambatana na kibaridi kikavu.
Kwa haraka sikutilia maanani sana kiupepeo hicho. Nilijua ni kawaida tu kwa sababu eneo hili halikuwa na miti mingi.
Lakini kwa dakika kadhaa upepo ulizidi kuvuma. Awamu hii upepo huo uliongeza kasi na ubaridi.
Nilibaini kuwa ulikuwa ukitokea upande wa mikorosho ya Mputa ambayo ilikuwa mita chache tu kutoka shambani kwangu.
Mara nikahisi mwili wote ukinisisimka huku nywele zikinisimama. Nilipata mshtuko ghafla. Mapigo ya moyo yakaanza kwenda mbio. Nguvu ziliniishia ghafla.
Ng’ombe nao wakasimama ghafla. Hapo ndipo nikahisi jambo la kuoghofya sana linaenda kutokea.
Ni kawaida ng’ombe kusimama pindi wanapokumbana na matukio ya kutisha. Huwa hawatembei kabisa hata uwaswage vipi.
Kutokana na hali hiyo ilinilazimu hata mimi pia kusimama ili kusikilizia nini kitatokea.
Naam! Nilipogeuka na kutaza upande wa kile kimsitu cha mikorosho ya Mputa, niliona moto mkubwa ukiwaka juu kabisa ya miti hiyo. Ulikuwa ni moto mkubwa sana.
Hata hivyo nilibaini kwamba moto huo licha ya kuwa mkubwa ulikuwa hauteketezi miti. Ulikuwa ni moto wa miujiza.
Ama kweli dunia hii inamambo na omba uyasikie tu kwa jirani lakini yasikutokee.
… USIKOSE SEHEMU YA PILI ITAENDELEA KESHO