Na Rashid Zahor
JUNI 15, mwaka jana, klabu kongwe ya Yanga iliandaa hafla maalumu na ya kihistoria, iliyopewa jina la ‘Kubwa Kuliko’, lengo lake kubwa likiwa kutoa nafasi kwa wanachama na wadau kuichangia timu hiyo.
Katika hafla hiyo, Yanga ilifanikiwa kupata zaidi ya sh. milioni 600, zilizotokana na michango ya fedha taslimu na ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali, zikiwemo kampuni zinazojihusisha kwa karibu na michezo nchini.
Kuandaliwa kwa hafla hiyo kulitokana na ukweli kwamba, Yanga ilikuwa na hali mbaya kifedha, ikiwa ni pamoja na kudaiwa mamilioni ya fedha na wachezaji wake, zikiwemo malimbikizo ya mishahara na fedha za usajili.
Vilevile, Yanga ilikuwa ikikabiliwa na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya na kuwaongezea mikataba mipya wale wa zamani, hali iliyosababisha viongozi kubuni tukio hilo ili kupata fedha za kutatua matatizo hayo.
Akizungumza katika tukio hilo, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliamua kuweka wazi mambo mengi kuhusu maendeleo ya mchezo wa soka nchini, uendeshaji wake na pia kushauri njia za kuikwamua klabu hiyo kutoka katika matatizo iliyonayo sasa.
Miongoni mwa ushauri alioutoa ni kuitaka Yanga kubuni mfumo mpya wa kuiendesha klabu hiyo kisasa, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika soka ya vijana kwa lengo la kuwaandaa wachezaji wa baadaye wa timu hiyo.
Rais huyo mstaafu, alisema mazoea yaliyojengeka hivi sasa kwa klabu za Tanzania, hasa Simba, Yanga na Azam, kusajili wachezaji wengi wa kigeni, badala ya wale wa ndani, yanachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha maendeleo ya mchezo huo kwa timu ya Taifa, Taifa Stars na pia kufifisha vipaji vya vijana.
Nimeikumbuka hotuba hiyo ya Rais mstaafu Kikwete katika hafla hiyo, kufuatia hali ya sintofahamu iliyoibuka hivi karibuni, baada ya uongozi wa Yanga, chini ya Mwenyekiti Mshindo Msolla, kutangaza kulivunja benchi lote la ufundi lililokuwa chini ya Kocha Mkuu, Cedrick Kaze.
Uamuzi wa Yanga kulivunja benchi la ufundi na kumfungashia virago Kaze, umekuja kwa kile kinachodaiwa timu hiyo kuanza vibaya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, hasa baada ya kufungwa mabao 2-1 na Coastal Union mjini Tanga na kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania mjini Arusha.
Matokeo hayo yamepunguza pengo la pointi kati ya Yanga na watani wao wa jadi Simba, ambao baada ya nao kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons mjini Dar es Salaam, watakuwa na uwezo wa kuipiku Yanga kwa tofauti ya pointi tano, iwapo watashinda mechi zao zote za viporo zilizosalia.
Yanga, imemtimua Kaze, raia wa Burundi, ikiwa ni miezi sita tangu alipoanza kuinoa timu hiyo, akiwa ameiongoza katika mechi 18, imeshinda 10, kutoka sare saba na kufungwa moja.
Klabu hiyo imeamua kumrejesha aliyekuwa Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi, ambaye aliomba kupumzika kwa madai ya afya yake kuwa siyo nzuri.
Mbali na Mwambusi, uongozi wa Yanga pia umeamua kumrejesha kocha wake wa viungo,
Edem Mortotsi kutoka Ghana, ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lililovunjwa.
Mghana huyo pamoja na Mwambusi wapo kambini na timu hiyo hivi sasa.
Uamuzi wa Yanga kumrejesha Mwambusi katika nafasi yake, umeacha maswali mengi. Wadau wengi wa soka nchini wamekuwa wakijiuliza iwapo ni kweli kocha huyo aliamua kupumzika kwa sababu za kiafya ama hakuwa akielewana na Kaze. Hiyo ni siri ya Mwambusi na Kaze.
Licha ya Yanga kumrejesha Mwambusi katika nafasi yake ya awali, imeshaweka wazi kuhusu mipango yake ya kulisuka upya benchi la ufundi, kwa kumleta kocha mkuu mpya kutoka nje ya nchi. Bado haijafahamika jina la kocha huyo na nchi anakotoka.
Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kuvunja benchi lake lote la ufundi. Iliwahi kufanya hivyo ilipokuwa chini ya Kocha Luc Eymael, aliyefukuzwa msimu uliopita, sanjari na aliyekuwa Kocha Msaidizi, Charles Boniface, aliyeamua kupumzika, Kocha wa Makipa, Peter Manyika, Meneja wa timu, Abeid Mziba na mtunza vifaa Fred Mbuna.
Pia, ilitangaza kuwaacha wachezaji 14, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kumaliza mikataba na wengine wakidaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu. Wachezaji walioachwa ni nahodha Papy Tshishimbi, David Molinga, Mrisho Ngasa, Jaffar Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vicent na Mohamed Issa. Pia, wapo waliositishiwa mikataba yao, Ali Mtoni, Muharami Issa, Ali Ali, Patrick Sibomana, Eric Kabamba, Rafael Daud na Yikpe Gislain.
Kilichodhihirika hadi sasa ni kwamba, pamoja na Yanga kusajili wachezaji kadhaa wapya na kubadili benchi la ufundi mara kwa mara, bado timu hiyo haijaweza kucheza katika mfumo unaoeleweka, badala yake kila mchezaji amekuwa akionyesha kipaji chake binafsi. Licha ya kuongoza ligi kwa muda mrefu, bado mashabiki hawajaridhishwa na kiwango cha soka kinachoonyeshwa na timu hiyo katika mechi zake.
Kibaya zaidi, mashabiki wa Yanga hawana subira na timu yao, hasa inapoteleza katika baadhi ya mechi. Ni wepesi wa kususa na kuishia kutoa lawama kwa viongozi na wachezaji, badala ya kuendelea kutoa hamasa kwa timu yao.
Ikumbukwe kuwa kikosi cha sasa cha Yanga kinaundwa na wachezaji wengi wapya waliosajiliwa msimu huu, hivyo kinahitaji kupata muda mrefu wa mafunzo ili waweze kucheza kwa uelewano na soka ya kuvutia. Katika hilo, maandalizi hayapaswi kuwa ya kulipua, yanahitaji muda wa kutosha na yawe ya kitaalamu.
Ni kosa kubwa kwa mashabiki wa Yanga kulazimisha timu yao icheze kama Simba, inayoshiriki katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika. Ni kwa sababu kikosi cha Simba kimedumu pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu na kiwango cha wachezaji wake wengi kipo juu ikilinganishwa na Yanga.
Ili kukabiliana vyema na matatizo yanayoikabili sasa Yanga, huu ni wakati mwafaka kwa klabu hiyo kutekeleza kwa vitendo ushauri uliotolewa na Rais mstaafu Kikwete, kuwataka viongozi wake wabuni mfumo mpya wa uendeshaji ili iweze kujitegemea, badala ya kutegemea zaidi misaada ya wafadhili.
Japokuwa kwa sasa Yanga ipo chini ya udhamini wa Kampuni ya GSM, kumekuwepo na mgongano na mwingiliano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya klabu. Baadhi ya wakati, viongozi wa GSM wamekuwa wakifanyakazi zinazopaswa kufanywa na viongozi, hivyo kuwafanya waonekane kama mapambo.
Vilevile, Yanga imekuwa ikipitia kipindi kigumu hivi sasa kutokana na kukosa mapato ya uhakika, hali inayosababisha iendeshwe kwa kutegemea michango ya wanachama na baadhi ya wafadhili. Katika hali hii, ni vigumu kuwashawishi mashabiki wafurike uwanjani kuishangilia kwa sababu hawana uhakika na uwezo wa timu yao.
Ili mashabiki wavutike kufika uwanjani, lazima timu iwe na wachezaji wengi wazuri na wenye kiwango cha hali ya juu, wanaolipwa mishahara kwa wakati na kukamilishiwa fedha za usajili bila kuwepo ‘bla bla’ yoyote.
Hapa ndipo ninapoukumbuka ushauri uliotolewa na Rais mstaafu Kikwete, kwa viongozi na wanachama wa Yanga kwamba, lazima wabadilike kwa kubuni mfumo mpya na wa kisasa wa kiundeshaji ili iweze kujitegemea na kuacha kutegemea michango ya wanachama na wafadhili.
Mabadiliko hayo yanapaswa kuanza mapema kwa uongozi uliopo madarakani kuhakiki idadi ya wanachama wake kote nchini, ili kujua rasilimali watu iliyonayo na kisha kuhakiki mali za klabu kwa lengo la kujua thamani yake na hatimaye kugeuzwa kuwa mtaji.
Pengine siyo vibaya kwa Yanga kuwaiga wenzao wa Simba, kubadili katiba ya klabu hiyo ili iruhusu kuwepo kwa kampuni, ambayo itakuwa chini ya wawekezaji watakaomiliki hisa nyingi, kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na serikali, huku wanachama nao wakiruhusiwa kununua hisa kupitia kiwango watakachowekewa.
Kutokana na mabadiliko ya nyakati yalivyo hivi sasa, mpango uliokuwepo awali wa kuikodisha klabu kwa mwekezaji ama mfanyabiashaya yeyote haufai, kwani unaweza kusababisha mgogoro wa kimaslahi. Kwa kuwa klabu ni mali ya wanachama, njia pekee nzuri ni kuunda kampuni na iendeshwe kwa mfumo wa kununua hisa.