Na NASRA KITANA
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo, kitashuka dimbani kupepetana na Kenya ‘Harembee Stars’, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.
Stars waliondoka juzi kuelekea nchini humo kwa ajili ya michezo miwili ya kujipima nguvu huku mchezo mwingine ukitarajiwa kupigwa Machi 18, mwaka huu, Uwanja wa Kisarani, Nairobi.
Stars watacheza michezo hiyo ikiwa ni maandalizi ya michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya Equatorial Guinea na Libya.
Akizungumzia mechi hiyo ya kirafiki, Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema mchezo huo ni muhimu kwao ili kuona ni jinsi gani kikosi chake kimepata maandalizi ya kutosha.
Amesema mchezao huo atautumia kuangalia kiwango cha wachezaji wote walioitwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON ikiwemo kurekebisha makosa ambayo yatajitokeza.
Kim amebainisha kuwa, anajua wachezaji wake kwa kipindi kifupi alivyokaa nao kwenye mazoezi, ameona ni jinsi gani ambavyo wamekuwa wakijituma na hiyo yote inampa nguvu.
“Najua Harembee Stars ni timu ngumu ya yenye changanoto za kotosha, ila mimi nakiamini kikosi changu kwa jinsi nilivyofanya maandalizi kuelekea mchezo huo, naamini tutashinda katika mechi zote mbili japokuwa tupo ugenini,” alisema Kim.
Kim ameongeza kuwa, mchezo huo ndio utampa majibu kamili ni wapi kwenye mapungufu ili aweze kuyafanyia kazi haraka kabla ya kucheza michezo miwili iliyobakia dhidi ya Guinea na Libya.
Kipa wa Stars, Juma Kaseja amesema kikosi chao kimekuwa na wakati mzuri wa kufanya mazoezi ya kujiandaa na michezo yao dhidi ya Kenya na ile ya kutafuta tiketi ya kufuzu AFCON.
“Tunajua mbele ya Kenya haitakuwa michezo rahisi kutokana na ukweli kwamba tunajuana vizuri, lakini kutokana na ari niliyoiona kwa wachezaji naamini tutafanya kitu kizuri na kupata ushindi,” alisema Kaseja.
Timu hiyo ipo kundi J ikiwa na pointi nne, ikiongozwa na Tunisia wenye pointi 10, Equatorial Guinea wanashika nafasi ya pili kwa pointi 6 na Libya inaburuza mkia kwa pointi zake tatu.
Stars itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Equatorial Guinea mchezo utakaopigwa Machi 25, mwaka huu ugenini, kisha watarejea nyumbani kuikabili Libya Machi 28, mwaka huu katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.