Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini(DCEA) wametoa mafunzo kwa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano ili kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya .
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo jijini hapa ,Kamishna wa kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema mafunzo hayo yatasaidia kufanikiwa kwa Programu ya TAKUKURU rafiki katika tatizo la dawa za kulevya na mapambano dhidi ya Rushwa kwa maafisa hao na kuleta matokeo chanya.
Amesema elimu ya kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya ikitiliwa mkazo zaidi mashuleni itasaidia kulinusuru kundi la watoto wenye miaka kati ya 10 hadi 12 ambalo kwa siku za hivi karibuni limetajwa kuwa hatarini zaidi kwenye uraibu wa dawa za kulevya.
“Rushwa na dawa za kulevya zinaingiliana, tumieni mafunzo mliyoyapata kutoa elimu kwa jamii na kuwapa uelewa ili kuongeza chachu ya mapambano na udhibiti wa madawa ya kulevya hivyo,tumeanza kwa wanafunzi ngazi za msingi,sekondari hadi vyuo vikuu hivyo kupitia klabu zao za kupambana na Rushwa watatumia pia klabu hizohizo kupambana na madawa ya kulevya , “amesema
