Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akizungumza wakati akifungua mafunzo kuhusu nafasi ya wahariri wa vyombo vya habari na Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga katika mapambano dhidi ya Rushwa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Jumatano Agosti 7,2024 katika ukumbi wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga yakilenga kujadili uzoefu, mchango wa vyombo vya habari katika kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na kuweka mikakati ya pamoja kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025
Kessy amesema TAKUKURU inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rushwa na madhara yake kwa sababu Tanzania inahitaji kuwa na wananchi wazalendo wasiojihusisha na vitendo vya rushwa.
“Nafasi ya vyombo vya habari katika kuzuia Rushwa kwenye uchaguzi ni kuhakikisha taarifa au habari ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi ya Tanzania inawafikia Watanzania, kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo rushwa, kushirikiana na TAKUKURU kwenye vita dhidi ya rushwa na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya rushwa kwenye uchaguzi”,ameongeza Kessy.