SERIKALI imeajiri watumishi wapya 16,676 wa kada za elimu na afya huku ajira 736 kwa upande wa afya zikikosa sifa, hivyo maombi ya kujaza nafasi hizo kutangazwa upya.
Kati ya ajira hizo mpya, waombaji 6,876 wameajiriwa katika kada za afya ambapo wanawake 3,217 sawa na asilimia 46.8, wanaume wakiwa 3,659 sawa na asilimia 53.2 na wenye ulemavu 42 wameajiriwa sawa na asilimia 0.61 kwa sababu ya uchache wa waombaji wenye sifa kutoka kundi hilo.
Akitangaza ajira hizo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, alisema nafasi 736 kada za afya zilikosa waombaji wenye sifa.
Alizitaja kada zilizokosa waombaji wenye sifa ni nafasi 50 za madaktari wa meno, nafasi 43 za matabibu wa meno, nafasi 244 za matabibu wasaidizi, nafasi 86 za mteknolojia mionzi na nafasi 313 za wauguzi ngazi ya cheti.
“Kada hizi zitarudiwa kutangazwa ili kupata waombaji wenye sifa watakaojaza nafasi hizo,” alieleza.
KADA YA UALIMU
Kwa upande wa kada za ualimu, Waziri Bashungwa alisema waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo kisha kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800, ambapo walimu 5,000 wamepangwa shule za msingi, walimu 4,800 wameajiriwa kwa ajili ya shule za sekondari, wakiwemo walimu wenye ulemavu.
Alisema kati ya walimu 5,000 wa shule za msingi, wanawake ni 2,353 sawa na asilimia 47.06 na wanaume ni 2,647 sawa na asilimia 52.94.
Alibainisha kwa upande wa walimu 4,800 wa shule za sekondari, wanawake ni 1,289 sawa na asilimia 26.85 na wanaume 3,511 sawa na asilimia 73.15.
Waziri Bashungwa alisema walimu wenye ulemavu 261 wa shule za msingi na sekondari wameajiriwa sawa na asilimia 2.66 ya walimu wote walioajiriwa wakiwemo wanawake 84 na wanaume 177.
“Napenda ieleweke, kwa walimu wa sekondari tumetoa ajira za walimu wa sayansi kwa asilimia 76 ya nafasi 4,800 tulizopewa,” alisema.
Awali, akifafanua maombi 165,948 yakiwemo ya wanawake 70,780 na wanaume 95,168 yaliyopokewa katika mfumo, alisema maombi ya kada za afya yalikuwa 42,558 na ualimu ni 123,390.
Alisema kwa sababu idadi kubwa ya waombaji, timu ya uchambuzi wa maombi ya ajira ilipewa vigezo vilivyoandaliwa vya mwongozo wa kutoa ajira kwa waombaji, lengo likiwa kuhakikisha uwepo wa haki na uwazi.
“Katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa, vigezo vilivyotumika kupata waajiriwa wapya kwa mwaka 2022, kila kigezo kilizingatia uwiano wa kijinsia,” alisema.
Alifafanua upangaji wa watumishi wa kada za afya na ualimu katika vituo vya kutolea huduma za afya na shule, umezingatia mahitaji ya watumishi katika mikoa husika.
“Kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya maboresho makubwa sekta ya afya, upangaji wa watumishi wapya umezingatia mahitaji ya watumishi katika halmashauri zenye hospitali mpya, vituo vipya vya afya na zahanati zilizokamilika ambazo zimeshindwa kutoa huduma za msingi, kwa kukosa watumishi wenye sifa,” alisema.
Kwa upande wa kada za ualimu, Bashungwa alisema utaratibu wa upangaji ulizingatia mgawanyo wa nafasi kwa kila somo na kiwango cha elimu kulingana na hitaji la kibali.
Alisisitiza mchakato huo umetoa fursa kwa waombaji kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, hivyo upangaji wake umezingatia uzalendo na utamaduni kwa kila Mtanzania kufanya kazi mahali popote nchini.
MAAGIZO
Alitumia nafasi hiyo kutoa maagizo yanayopaswa kuzingatiwa na waajiri na waajiriwa ambapo aliwataka waajiriwa wapya wahakikishe wanaripoti kwa wakurugenzi wa halmashauri walizopangiwa wakiwa na kitambulisho cha taifa au namba ya utambulisho ya NIDA, cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti halisi vya taaluma na utaalamu wa kazi vya mwajiriwa, ili vihakikiwe.
Pia, aliwataka waajiri kuhakikisha wanapokea vyeti na kuviwasilisha Baraza la Mitihani (NECTA) kwa uhakiki na wizara ipewe taarifa kwa watakaokutwa na vyeti vya kughushi ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Waziri huyo aliagiza waajiri wahakikishe watumishi wapya waliopangwa katika halmashauri, wanapewa barua za ajira kisha kuripoti katika vituo walivyopangiwa na siyo vinginevyo.
Vilevile, alisema waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14, kuanzia tarehe ya tangazo watakuwa wamepoteza nafasi zao ambazo zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo katika kanzidata ya Ofisi ya Rais–TAMISEMI.
Katika hatua nyingine, Bashungwa aliwaelekeza wakuu wa shule na walimu wakuu kushirikiana na bodi za shule kufuata miongozo ambayo wizara imetoa kwa ajili ya michango ya wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Na SELINA MATHEW, Dodoma