MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Dk. Tito Mwinuka, amesema njia mbadala ya kununua umeme kwa mwananchi anayepata changamoto ya kununua kupitia Mfumo wa Kuuza Umeme wa Malipo ya Kabla (LUKU),ni kujaribu mtandao zaidi ya mmoja na kupitia huduma za kibenki.
Dk. Mwinuka ameyasema hayo leo, alipokutana na waandishi wa habari kutolea ufafanuzi jinsi TANESCO inavyojipanga kuondokana na changamoto ya kukosekana kwa mfumo wa LUKU na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.
Mkurugenzi huyo amesema, kwa sasa TANESCO wanafanya kazi ya kuimarisha mfumo wa LUKU kwa kuuongezea mfumo mbadala (backup), hivyo wakati majaribio ya mfumo huo yanapofanyika, kuna uwezekano wa kuwepo kwa changamoto za manunuzi ya nishati hiyo.
“Hivi sasa tunaendelea na kazi ya kuhamisha taarifa kutoka kwenye mfumo wa msingi kupeleka kwenye mfumo mbadala baada ya kuukamilisha kuujenga,” amesema Dk. Mwinuka.
Mkurugenzi huyo amesema, mfumo huo wa LUKU ulianza kufanya kazi Mei 19, 2021 mchana, baada ya kutokea kwa hitilafu ya manunuzi ya umeme Mei 17 na 18, mwaka huu na hivi sasa kazi ya kujenga mfumo mbadala inaendelea.
Kadhalika, amesemq katika kipindi hicho cha maboresho ya mfumo, kutakuwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika manunuzi ya umeme kutokana na majaribio yanayoendelea katika mfumo mbadala.
Na Pius Ntiga