Na Gift Mongi, Monduli
BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), imesema inasambaza tani 225 za mbegu bora za ngano kwa wakulima wa wilaya tano kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Aidha, bodi hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya kuzalisha na kusambaza mbegu ya Seed Co Tanzania, zimeahidi kutoa elimu na usaidizi wa kitaalamu kwa wakulima kwenye maeneo hayo ili kuwawezesha kupata mavuno mengi na bora.
Meneja wa CPB, Kanda ya Kaskazini, Hiza Kiluwasha, alikabidhi tani 17 za mbegu hizo kwa uongozi wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Ngano Monduli Juu (AMCOS), kwa lengo la kukuza uzalishaji wa zao hilo.
Mbegu hizo zilipokelewa na viongozi wa ushirika huo, akiwemo Mwenyekiti, Moloimeti Sane na Katibu, Sifael Lormunyoi na kuhifadhiwa kwenye ghala la Kijiji cha Emairete, kilichoko Kata ya Monduli Juu, tayari kusambazwa kwa wakulima.
Imeelezwa kuwa mbegu hizo za ngano ya chakula, zina ubora wa hali ya juu kutokana na kuwa na protini ya kutosha, hivyo ngano itakayovunwa, inafaa zaidi kwa matumizi ya nyumbani na viwandani, ambako hutumika kutengeneza mikate, keki, chapati na vyakula vingine.
“Tuna faraja kubwa sana kuletewa mbegu ya ngano na mbegu hii hatujawahi kuiotesha, hivyo tutajitahidi kuwa makini sana wakati wote wa kilimo cha ngano hii ya chakula, kuanzia ikiwa shamba mpaka kuvuna ili tuweze kujua ubora wake.
“Tunataka tufanye vizuri ili tuondokane na adha ya kilimo cha shayiri, ambacho tumedumu nacho kwa muda mrefu, lakini kwa sasa soko linayumba,” alisema Sane.
Aliishukuru serikali kwa kuwasaidia kwenye zao la ngano ya chakula, ambalo lina bei ya uhakika kuliko mazao mengine wanayolima .
Katibu wa AMCOS, Lormunyoi alisema kitendo cha CPB, kuingia nao mkataba wa kununua ngano yote watakayoivuna, kimewapa faraja kwa kuwa wanalima wakiwa na uhakika wa kuuza mazao yao kwa bei nzuri.
Meneja wa CPB, Kanda ya Kaskazini, Kiluwasha, alisema ngano hiyo imesambazwa kwenye maeneo, ambayo wameishaingia mikataba na wakulima kwa ajili ya kununua ngano yao pindi wakivuna.
Alisema hilo linatekelezwa kanda ya kaskazini, ambako tayari wameshakabidhi mbegu hizo za ngano kwa wakulima wa Nangwa, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, Karatu na Monduli Juu, mkoani Arusha na West Kilimanjaro, Wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.
“Tutahakikisha wakulima tulioingia nao mkataba wote wanapata mbegu na Jumatatu (leo), wote watakuwa wanapanda mbegu hizo shamba. Hii ngano ni ile yenye ubora, imekidhi viwango, itaanza kupandwa Jumatatu. Tunatekeleza maagizo ya Rais Dk. John Magufuli, kuhakikisha zao la ngano linafufuliwa na tunahamasisha wakulima wengi kulima,” alisema.
Alisema CPB imeingia makubaliano ya kimkataba na wakulima wa Monduli Juu, kuhakikisha wanapolima, wanawapatia mbegu na wanapovuna wananunua ngano yao yote.
Kiluwasha, alisema wameshirikiana na Kampuni ya Mbegu ya Seed Co Tanzania, kuagiza mbegu hizo zinazozalishwa na kampuni hiyo nchini Zambia, ambazo wanawauzia wakulima kwa sh. 2,900, kwa kilo moja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Seed.Co, ukanda wa Afrika Mashariki, Clive Mugadza, alisema kampuni yake italeta wataalamu wake wawili watakaopita kwenye maeneo ya mashamba ya wakulima waliouziwa mbegu hizo ili kuwapatia elimu na ujuzi zaidi juu ya namna bora ya kulima ngano hiyo, ili iwe na matokeo mazuri.
Aliwashukuru CPB na serikali kwa kuiamini kampuni yao na kufanya kazi pamoja huku akisifu namna taasisi nyingine za serikali zinazohusika na kuangalia ubora, likiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa kazi waliyoifanya na kuhakikisha mbegu zinawafikia wakulima kwa wakati.