MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la zao la Mchele Tanzania, Winnie Bashagi, amesema taifa ina akiba ya ziada ya mchele zaidi ya tani milioni 2.1.
Akizungumza na UhuruOnline, Winnie, amesema tangu mwaka 2007 serikali iliacha kuagiza mchele kisha kuimalisha kilimo cha mpunga nchini ambapo wakulima walihamasika na kuongeza uzalishaji.
Alisema kila mwaka taifa limekuwa likizalisha kiasi kikubwa cha mchele, hivyo ni wakati wa kufanya biashara ya zao hilo nje ya nchi.
“Tangu mwaka huo 2007 taifa hatukuhitaji kuongezea mchele kutoka nje ya nchi kwani kiasi tunachozalisha ni kingi na kinatutosheleza kwa chakula na ziada,” alisema.
Alibainisha kuwa Tanzania imekuwa nchi ya nne kwa kuzalisha kwa wingi zao la mpunga ikitanguliwa na Nigeria, Misri na Madagascar.
Alieleza kuwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati yamekuwa yakitegemea mchele unaozalishwa Tanzania kwa kiasi kikubwa.
Winnie alisema kwa sasa mchele umekuwa ni zao la biashara ambapo baraza hilo limekuwa likisisitiza mchele kama dhahabu nyeupe kwani umekuwa na soko kubwa kimataifa.
“Changamoto iliyopo kwa sasa ni kuhusu mfumo mzuri wa soko la mpunga hasa kwa kutojua namna bora ya uuzaji wa mchele. Mfumo haujawa sawa, bado tunashughulikia ziada iuzweje na kwa namna gani, hilo ndio suala kuu,” alibainisha.
Naye, Ofisa Programu wa Baraza la Mchele Tanzania, Geofrey Rwiza, alisema ili kusafirisha mchele katika soko la nje, inabidi kuzalisha mchele bora wenye viwango vinavyotakiwa.
Rwiza alijata sifa zinazohakikiwa ili kukidhi ubora wa kimataifa wa mchele ni kuepuka mchanganyiko wa mbegu katika aina moja ya ujazo, kuepuka uwepo wa vitu visivyohusiana na mchele katika ujazo na kuepuka kiasi kikubwa cha uvunjikaji wa mchele.
Na SCOLASTICA MSEWA, Dar es Salaam