Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) imeshiriki mpango wa “Hand in Hand” kwa utaratibu wa kujikita zaidi kwenye kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa malengo ya kupunguza umaskini na kuzuia njaa kwa wananchi wa Tanzania yanafikiwa.
Katibu Mkuu Mweli amesema hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa mpango huo unaoratibiwa na FAO uliofanyika jijin Dar es Salaam leo tarehe 29 Septemba 2023.
Katibu Mkuu Mweli amesema ili kufikia malengo ya mpango huo, Serikali imekuwa ikiwaonesha wawekezaji fursa zote zilizopo kwenye sekta ya kilimo Tanzania. Amefafanua kuwa kabla mwekezaji hajafika Tanzania huoneshwa fursa kama vile ardhi, maji, miundombinu ya usafirishaji pamoja na tathmini za kifedha na kiuchumi.