Bodi ya Ligi imetangaza marekebisho na maboresho ya kanuni toleo la 2023 ambapo hivi sasa ikiwa mchezaji ataingia makubaliano na benki nyingine tofauti na NBC basi hataruhusiwa kutangaza.
Katika marekebisho hayo, mchezaji atakayekiuka atakabiliwa na kufungiwa kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja na mpaka mitatu.
Kwa mujibu wa kanuni namba 16: 1:12 katika maboresho; “Hairuhusiwi kwa mchezaji kuingia mkataba binafsi wa udhamini na mshindani wa kibiashara wa Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu, atakayekiuka atafungiwa kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja na mitatu”
Akitoa maoni yake, Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga Simon Patrick ambaye ni mmoja wa Wanasheria wa FIFA, amesema kanuni yoyote kwenye mikataba ya kibiashara hutengenezwa kwa manufaa ya mpira, timu na wachezaji.
“Kama waliopitisha hii kanuni wameona ina maslahi kwa wachezaji wetu na mpira kwa ujumla wake, basi sawa! Si vibaya tukaiga mambo mazuri kwa wenye soka lao, wenzetu sikuhizi hawatoi tena exclusive rights kwa wadhamini,” aliandika Simon kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.
Ni wazi mabadiliko haya yanakwenda kuwaathiri Stephane Aziz Ki na Farid Mussa ambao waliingia mikataba na benki ya CRDB.