Na SUPERIUS ERNEST
WATANZANIA wametakiwa kuepuka vitakasa mikono (senitizer), ambazo hazijathibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), ili kuepuka madhara.
Vitakasa mikono ambavyo havijasajiliwa na TMDA havina ubora kutokana na sababu mbalimbali ikiwame baadhi kuzidishwa kiwango cha kilevi (alcohol) ambayo husababisha mikono kuchubuka au kupasuka.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Mchunguzi wa maabara ya TMDA, Gerald Sambu, amesema kutokana na uhitaji mkubwa wa bidhaa hiyo, baadhi ya wafanyabishara wametengeneza vitakasa mikono visivyokuwa na ubora kwa afya.
“Ili kuepuka athari hizo ni vyema kila mtu anapoenda kununua vitakasa mikono akawa makini kujiridhisha kama vimesajiliwa na TMDA ,” Gerald Sambu
Amesema wananchi wanatakiwa kuzingatia tarehe ya kumalizika matumizi kwa vitakasa mikono jambo ambalo linaweza kuwaepusha kutumia senitizer zilizopitwa na muda.
“Wanatakiwa kuangalia vitakasa mikono ambavyo vipo kwenye hali ya kimiminika, ambavyo havija ganda sana, vingine vimeganda kama mafuta ya kupaka, hivyo siyo vizuri kwa matumizi,”
Sambu amebainisha kuwa, kitakasa mikono kizuri ni kile kisicho wahi kukauka au kisichochelewa kukauka mikononi baada ya kupaka.
Mchunguzi huyo amesema senitizer nzuri ni ile yenye kipimo cha kutambua kiwango cha asidi na besi (PH 6-8), hivyo ikiwa chini ya hapo au kuzidi haifai kwa matumizi.
Mchunguzi huyo ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), vitakasa mikono bora ni vile vilivyotengenezwa kwa kutumia kilevi ingawa vingine vinatumia kemikali.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa TMDA, James Ndege, amesema zipo senitaiza nyingi ambazo zimeshasajiliwa na TMDA na wanaendelea kufanya hivyo.
Ndege amewataka wafanyabiashara ambao hawajasajili senitizer zao kuhakikisha wanazipeleka TMDA kuzifanyia ukaguzi na usajili kwa sababu wakibainika wanauza bila utaratibu watachukuliwa hatua za kisheria.
MAONI YA WANANCHI
Jafari Kibasila, mkazi wa Mbagala Sabasaba, Dar es Salaam, amesema kwa kuwa hivi sasa vitakasa mikono imekuwa bidhaa muhimu katika maisha ya kila siku kutokana na tatizo la ugonjwa wa covid-19, ni vyema mamlaka husika zikatoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa kuzibaini zisizofaa kwa matumizi.
“Senitaiza kwa kipindi hiki ni kama bidhaa ya lazima kwa kuwa yapo baadhi ya maeneo ya kutolea huduma unalazimishwa kupaka kabla ya kuhudumiwa, sasa ni muhimu elimu ikatolewa ili kila mmoja aweze kuzing’amua zisizo na ubora stahili,” Jafari Kibasila.
Zainabu Rajabu, Mamalishe anayefanya shughuli zake katika soko la Feri, aliiomba TMD na mamlaka zingine zinazosimamia ubora wa bidhaa hiyo, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kuwa ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuweza kupambanua iliyo bora na isiyo na ubora.