SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limeanza kutoa elimu ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, kwa wananchi waishio maeneo ambako mradi huo unapita Mkoani Mwanza, ikiwa ni kipande cha tano ili kutimiza lengo la uendelezaji wa miundombinu ya reli nchini.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mkoa ea Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amesema kampeni hiyo inalenga kutoa uelewa kwa wananchi juu ya changamoto zinazowaweza kujitokeza wakati wa ujenzi wa mradi na namna ya kuzitatua pindi zitakapojitokeza.
“Kupitia elimu hii, wananchi watapata uelewa juu ya ujenzi wa reli, utunzaji wa mazingira, utaratibu wa kufuata namna ya kutwaa ardhi, matumizi bora ya fedha za fidia, faida ya miradi ya kimkakati na historia ya taifa, kuwaelimish na kutambua fursa zinazotokana na miradi ili washiriki katika nyanja mbalimbali,” amesema Mhandisi Gabriel.
Aidha, amesema katika ujenzi huo, wananchi wote watakaopitiwa na mradi huo watalipwa fidia zao kwa kulingana na sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999 na hakuna ambaye haki yake itapotea.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, ujenzi wa Reli kutoka Mwanza hadi Isaka ni Kilomita 341, ambapo unatarajia kutoa ajira 11,000 na kwamba kwa Mkoa wa Mwanza, unayagusa moja kwa moja maeneo ya Nyamagana, Kwimba, na Misungwi.
Na Johari Shani



























