RAIS Samia Suluh Hassan, amewataka wanawake kufanya kazi kwa bidii na kutokuwa wavivu katika kuchangamkia fursa zilizotokana na mabadiliko ya wimbi la ugonjwa wa Uviko-19.
Amesema kutokana na kutulia kwa wimbi hilo duniani, kumeanza kujitokeza mageuzi ya kiuchumi ikiwemo fursa mbalimbali kufunguka.
Kauli hiyo aliitoa katika maadhimisho ya sherehe ya Siku ya Wanawake Duniani, ambazo kitaifa zilifanyika katika uwanja wa Maisara mjini Unguja.
“Tumeanza kuona ishara ya kuwa ukizunguka duniani unakuta mazao ambayo sisi Tanzania tunalima na tunasema ndiyo chakula na siyo mazao ya biashara, sasa ndiyo maisha ya biashara,” alisema.
Alisema katika maeneo mbalimbali duniani, bidhaa za kilimo ikiwemo mchele, mboga na mazao ya mifugo hususan nyama ambayo inazalishwa kwa wingi nchini, vinahitajika kwa wingi.
“Sasa kwa maana hiyo kuna soko kubwa la vyakula, bidhaa hizo zikiwemo mbogamboga na mambo mengine. Nayasema hayo kuonyesha fursa iliyotolewa na mabadiliko ya ugonjwa wa Uviko – 19, kazi inayotukabili sisi wanawake ni fursa iliyopo,” alisema.
Alisema fursa hiyo itawafaidisha wanawake iwapo watasimama imara, kushikamana huku wakiamini kufanikiwa kupitia fursa zinazojitokeza.
Aliwataka wanawake kuchangamkia fursa za kiuchumi katika kufikia maendeleo ya kweli na wanapaswa kushikana mikono kuendeleza harakati za maendeleo nchini.
Rais Samia alieleza lengo la siku ya wanawake duniani ni kujitathmini kwa waliyofikia, wapi walipo, wanapoelekea na kuangalia changamoto zinazowakabili katika kuweka mikakati ili kuziondosha na kuleta maendeleo.
Alieleza msingi wa taifa lolote ni familia, hivyo maadhimisho hayo ni fursa ya kutathimini utekelezaji wa maazimio, mikataba na makubaliano ya kikanda, kimataifa na yale waliyotunga kwa kiasi gani yametekelezwa na mafanikio yaliyopatikana, lengo kuu likiwa ni kumkomboa mwanamke.
Pia, alisema serikali zote mbili zimedhamiria na zinatekeleza mikataba na maazimio ya kikanda, kimataifa na waliyojiwekea, ambayo yanalenga kuhakikisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake unafikiwa ifikapo mwaka 2030 kimataifa na 2063 katika bara la Afrika.
Aidha, Rais Samia alisema uridhiaji na utekelezaji wa mikataba ya mazimio hayo, ni ushahidi kwamba taifa linaunga mkono jitihada za kimataifa za kukuza usawa wa kijinsia na serikali zimekuwa zikifanya hivyo ili kufikia kizazi chenye usawa kwa maendeleo ya nchi.
Alisema ili mwanamke akomboke kiuchumi, ni lazima kumpatia ujuzi, hivyo serikali inajenga vituo vya amali na maendeleo ya jamii ili kutoa fursa kwa wananchi kupata mafunzo kwa ajili ya kuongeza ujuzi ili bidhaa zao zikubalike katika masoko.
Pia, alisema serikali zote mbili zimeanzisha mifuko na majukwaa ya kuwawezesha wanawake na tayari wamefanyia kazi kwa kuona inaweka mtaji kila mkoa ili kuwawezesha wanawake.
UMUHIMU WA SENSA
Akizungumzia kuhusu Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, Rais Samia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuhesabiwa.
“Hata kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Wanawake Duniani kwa upande wa Tanzania Bara inasema jitokeze kuhesabiwa, hivyo niongeze sauti yangu kwa kusema tujitokeze kuhesabiwa,” alisema.
Alisema sensa inafanyika kwa lengo la kujua idadi ya wananchi wa Tanzania na kusema kuwa kuna propaganda zinapitishwa kwamba sensa ya mwaka huu watu wataulizwa kuhusu dini zao jambo ambalo siyo la kweli.
Rais Samia aliwahakishia wananchi kuwa, suala hilo halipo kwa kuwa lilishakataliwa na Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambapo alikataza kuulizana udini.
“Sensa zote ambazo zimewahi kufanyika Tanzania, jambo hili halijawahi kutokea, sasa nashangaa wale waliozusha kipindi hiki na kusema sensa mwaka huu itakwenda kuuliza watu dini zao, nataka kuwahakikishia kuwa hilo halipo,” alisema.
Alisema kilichoongezeka katika sensa ya mwaka huu ni kujua anwani za makazi za wananchi na wameanza na hilo ili sensa ifanyike vyema.
“Tunataka kujua na kuona kwenye ramani zetu tutakazozichukua kidigitali tuone maeneo ambayo hayatahesabiwa na maeneo ambayo maafisa waliopangiwa kazi watayaruka, sisi tunataka kuhakikisha kwamba watu wote wamehesabiwa,” alisema.
Rais Samia aliwataka wananchi wote kujitokeza kuhesabiwa na kutoa ushirikiano mkubwa katika anwani za makazi kwa sababu hilo halitakuwa na maana kwenye sensa peke yake bali litakuwa na maana pia katika mambo mengi.
HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR



























