Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume leo tarehe 19 Desemba, 2023 jijini Dodoma.
“Hongereni sana kwa kuendesha vizuri zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mlilolifanya kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023. Tumeona mmejipanga na mpo tayari kwa uboreshaji,” amesema Mhe. Nderiananga ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Baraza hilo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi,Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ambayepia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima alilijulisha Baraza hilo kwamba uboreshaji wa majaribio umefanyika kwa mafanikio.
Bw. Kailima amesema katika uboreshaji huo wa majaribio, Tume ilifanikiwa kupima uwezo wa vifaa na teknlojia ya uboreshaji ambalo ndilo lilikuwa lengo kuu la zoezi hilo.
“Tumefanikiwa kupima uwezo wa vifaa na teknolojia japo hatukupata watu waliotumia mfumo wa kujiandikisha kwa njia ya mtandao. Changamoto tumezigundua na tunazifanyia kazi kwa ajili ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari,” amesema Bw. Kailima.
Tume ilifanya uboreshaji wa majaribio kwenye Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora kwa siku saba kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Katika hatua nyingine, Mhe. Nderiananga amewaasa wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana, kuepuka mambo ya utovu wa nidhamu na kudumisha utamaduni wa kujengeana uwezo wa kiutendaji.
“Mnayo nafasi kubwa katika kuwahamasisha watumishi wenzenu ili waweze kuwa na ufanisi kazini, ufanisi huo utatokana na ushirikiano mzuri kati ya watumishi na viongozi,” amesema.
Mhe. Nderiananga amesisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kuitisha mabaraza ya wafanyakazi kwa kuwa ni jambo la kisheria na linalolenga kuweka mazingira mazuri na ustawi wa wafanyakazi.





























