WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha amani, ushirikiano, ustawi wa kijamii na kiuchumi unaendelea kushamiri katika nchi zote za Bara la Afrika.
Ameyasema hayo (Alhamisi, Februari 24, 2022) alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
Amesema katika kuhakikisha inashiriki kwenye ukuzaji wa ustawi wa kiuchumi barani Afrika, Tanzania inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa kutoka uvinza (Tanzania)- Gitega (Burundi) hadi Kindu (DRC).
“Pia tunajenga SGR kutoka Isaka (Tanzania) hadi Kigali (Rwanda)” Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa mradi mwingine unaolenga kukuza uchumi wa Afrika ni pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanzania).
Kadhalika, Majaliwa amependekeza kuwa katika mikutano mingine ya nchi wanachama wa Makubaliano ya Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC na Ukanda wa Maziwa Makuu Lugha ya Kiswahili iongezwe kama mojawapo ya lugha rasmi ya mikutano hiyo.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo Waziri Mkuu Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa DRC Tshisekedi ambapo pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara.
Waziri Mkuu amesema Rais Tshisekedi ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini DRC.
Viongozi wengine aliofanyanao mazungumzo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya amani Jean-Pierre Lacroix.
Pia, Waziri Mkuu alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Burundi, Evariste Ndayishimiye ambapo pamoja na mambo mengine walijadiliana namna ya kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na kuimarisha uchumi.