TIMU ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’, imezidi kutakata baada ya kuichapa Sudan Kusini kwa mabao 3-0, katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi wa michuano ya Shirikisho la Vyama Vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA).
Twiga Stars iliibuka kidedea katika mchezo wa tatu wa kundi B, uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela Bay, Jijini Port Elizabeth nchini Afrika Kusini.
Katika mchezo huo mshambuliaji Stumai Abdallah, alipiga ‘hat trick’, ambapo alikwamisha mabao wavuni katika dakika za 52, dakika ya 80 na bao la tatu akifunga muda mchache kabla ya mchezo kumalizika.
Twiga Stars tayari imeshatinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo baada ya kupata ushindi wa michezo yake yote mitatu, ikianza dhidi ya Botswana 2-0 akaibamiza 3-0 Botswana kabla ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Sudan Kusini.
Katika ya nusu fainali itakayochezwa keshokutwa, Twiga Stars itapepetana na mshindi kati ya Zambia na Uganda ambaye atapatikana leo baada ya kumalizika mechi ya mwisho ya makundi ya kundi C.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha wa timu hiyo Bakari Shime alisema amefurahi kuona wamemaliza hatua ya makundi wakiwa kileleni mwa msimamo wa kundi B ambapo wamejikusanyia pointi tisa.
Alisema walijipanga vyema ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechezo huo, kitu ambacho wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kwa sasa wanaanza maandalizi ya mechi inayofuata ya hatua ya nusu fainali na watahakikisha wanapambana ili kuibuka na ushindi mnono.
Alisema mechi ya nusu fainali haitakuwa rahisi kwani kila timu imejipanga kusonga mbele, lakini ana imani ya kukipanga vyema kikosi chake kwa ajili ya kuibuka na ushindi.
“Michezo ilikuwa migumu kwa pande zote lakini ninashukuru Mungu wachezaji wangu wameweza kufuata kile ambacho nimewafundisha na kufanya vyema katika michezo yote, sasa malengo yetu ni kushinda mchezo wa nusu fainali na kutinga fainali ya michuano hiyo,” alisema Shime.
Shime aliwataka Watanzania kuendelea kutoa sapoti kwa timu yao ili iweze kufanya vizuri katika mechi inayofuata na fainali.
Mchezaji bora wa mechi hiyo Stumai, alisema wamefurahi kumaliza kundi wakiwa wanaongoza na kushinda michezo yote mitatu kwani kila mchezaji alionyesha kujituma kuipambania timu.
“Sisi kama wachezaji tunafuata mafundisho ambayo mwalimu anatupa na kuyafanyia kazi, ndio maana tunashinda katika kila mchezo na haya ndio malengo yetu hatuna sababu ya kushindwa kurejea nyumbani na ubingwa,” alisema Stumai.
Na MWANDISHI WETU