MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Oktoba 19, mwaka huu, inatarajia kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake.
Uamuzi huo ni ule unaohusu kupokelewa au la kwa maelezo ya onyo yanayodaiwa kutolewa na mshitakiwa Adam Kasekwa.
Mbali na Mbowe na Kasekwa, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi ni Alfani Bwile na Mohamed Ling’wenya.
Jaji Mustafa Siyani anayesikiliza shauri hilo, amepanga kutoa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, baada ya Wakili wa mshitakiwa Kasekwa, John Malya kuieleza Mahakama kuwa, hawana shahidi mwingine, hivyo ameufunga ushahidi wao.
Aliwataka mawakili wa pande zote katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi, Oktoba 4, mwaka huu, wawasilishe hoja zao za mwisho kwa muhtasari zisizozidi kurasa tano, zikiwa na mambo muhimu, waambatanishe na sheria na uamuzi utakaomsaidia katika kutoa uamuzi.
Baada ya kueleza hayo, Jaji Siyani aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi na kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Na REHEMA MOHAMED



























