Na RESTITUTA MARTIN.
UBALOZI wa Japani umetoa bilioni 3.1 kwaajili ya kuboresha miundombinu ya soko la samaki la Malindi lililopo visiwani Zanzibar.
Makubaliano ya utoaji wa fedha hizo ulisainiwa juzi katika ofisi ndogo za serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilizopo Posta Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali alisema kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo utawapa fursa wananchi wa visiwani humo kujiendeleza kiuchumi.
Aidha Waziri Ali alisema awali soko hilo lilishindwa kukamilika kwasababu lilikuwa kwenye uneo la hifadhi ya jamii na hivyo walikuwa wakifanya juhudi za kutafuta kibali cha ujenzi.
“Ni matarajio yetu sasa baada ya kusaini makubaliano haya mradi huu utaanza haraka na kumalizika kwa wakati, nikwasababu soko hilo linaumuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa Serikali na kwa uchumi wa wananchi” alisema.
Waziri Ali alisema hapo awali ujenzi wa soko hilo ulikwama kwa kipindi kirefu na hivyo baada ya kupata msaada huu hakuna kingine kitakachiokwamisha ujenzi huo ambao unatarajia utafanyika ndani ya kipindi kifupi.
Waziri Ali alisema Japan ni wadau muhimu katika maendeleo ya Zanzibar na hivyo wataendeleza uhirikiano kati ya nchi hizo mbili katika mambo muhimu yanayoleta maendeleo na tija kwa wananchi.
Aidha Waziri Ali aliwatakaa wawekezaji kutoka taasisi binafsi kujitokeza ili kuwekeza katika sekta ya utalii visiwani humo kwani serikali imeshatenga maeneo maalumu kwaajili ya uwekezaji.
Kwa upande wake Naibu balozi wa Japan Tokashi Niinuma alisema Japan ina malengo mazuri ya kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya nchi yake na Tazania ikiwa ni pamoja na kutoa misaada mbali mbali kwaajili ya miradi ya maendeleo.
Balozi Niinuma alisema baada ya kusaini mkataba huo wakandarasi wataanza ujenzi wa soko hilo mara moja ili kukamilisha mradi huo maalum kwaajili ya kuwanufaisha wavuvi na wafanyabiashara wa Samaki.
“Kama ilivyo huku nchini kwenu hakuna “lock down” na sasa baada ya kusaini mkataba huu tutahakikisha wakandarasi wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huu mara moja” alisema.



























