VITA ya nani kipa mwenye kiwango bora katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Aishi Manula na Djigui Diarra, umewaibua wakongwe wa soka nchini ambao wametaja sababu za msingi za kumtambua kipa bora.
Licha ya makipa hao, wengine ni Haroun Mandanda wa Mbeya City ambaye hajaruhusu bao katika mechi tatu sawa na Hussein Masalanga wa Dodoma Jiji.
Pia wamo Metacha Mnata wa Polisi Tanzania akiwa hajaruhusu bao katika mechi mbili sawa na Hamad Kadedi wa Mbeya Kwanza.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, kipa wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Ivo Mapunda, alisema kipa mzuri anapimwa na kigezo cha kutoruhusu bao katika mechi.
Mapunda alisema baada ya kipimo hicho, ndio vinafuata aina ya hatari alizookoa ukiwemo uwezo wake binafsi akiwa langoni.
“Kwanza anapimwa kwa idadi ya mechi ambazo hajaruhusu mabao, pili aina ya hatari alizookoa na uwezo wake. Manula na Diara wote ni bora katika timu zao, kila mtu anasaidia kutokana na timu aliyokuwa nayo,” alisema.
Kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay, alisema katika mechi tano zilizochezwa, kwake anaamini Manula ndiye kipa bora zaidi ya wengine kutokana na kigezo cha kutoruhusu bao lolote.
“Vitu vingi vya kuangalia, kutoruhusu mabao, lakini dakika alizocheza, alafu baadae ndio hatari alizookoa, kwangu, Manula anamuongoza Diarra.” alisema Mayay.
Naye kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema kigezo namba moja cha kipa bora ni kutoruhusu bao katika mechi na ndicho kinachomfanya aamini katika mechi tano zilizopita, Manula alikuwa bora zaidi ya Diara.
“Namna anavyolinda lango lake, kuzuia bao lisipatikane, kipa bora ni yule ambaye amefanikiwa kuzuia bao lisipatikane, kwa hiyo, kati ya hao makipa, Manula anawaongoza wenzie katika mechi hizi tano za kwanza,” alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 15 baada ya kushinda mechi zote tano ikifuatiwa na Simba yenye pointi 11 wakati Polisi Tanzania ikishika nafasi ya tatu kwa pointi kumi sawa na Dodoma Jiji katika nafasi ya nne.
Na ABDUL DUNIA