SERIKALI ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo (AFD), imetia saini mkataba wa kuipatia Tanzania mkopo wa Euro milioni 75 (sh. bilioni 195), kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Usambazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo jijini Dar es Salaam, jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, alisema lengo la mradi huo ni kutoa huduma za uhakika na endelevu za upatikanaji maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Shinyanga.
Tutuba alisema mradi huo utaboresha afya, ustawi wa jamii na hali za maisha ya wanufaika wake kwa kuboresha na kuimarisha miundombinu iliyopo, kuongeza ufanisi wa uendeshaji na utoaji huduma bora kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA).
“Hii ni ajenda kubwa inayoendana na hatua za serikali, kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaotoa vipaumbele na kuboresha upatikanaji na usambazaji maji na huduma za usafi wa mazingira mijini na vijijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira na ufadhili huu wa AFD utachagia kufikia moja ya vigezo vya mpango huo wa kuongeza asilimia ya watu wa mijini wanaopata huduma ya maji safi,” alisema.
Tutuba alieleza mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji maji safi na salama kwa asilimia 95 katika Manispaa ya Shinyanga na baadhi ya miji midogo katika Wilaya ya Shinyanga na kunufaisha wananchi zaidi ya 306,566.
“Uzalishaji wa maji utaongezeka kutoka mita za ujazo za sasa ambazo ni 25,877 kwa siku, hadi 33,944; na kuongeza nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika maeneo yanayozunguka mradi,” alisisitiza Tutuba.
Katibu Mkuu Tutuba alizitaka taasisi zitakazotekeleza mradi huo (Wizara ya Maji na SHUWASA) chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Sanga, watumie uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Sekta ya Maji Tanzania, Programu ya Huduma Endelevu za Maji na Usafi wa Mazingira vijijini na miradi mbalimbali ya maji iliyofadhiliwa na AFD ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Shinyanga na nchi kwa ujumla.
Aliihakikishia Ufaransa kwamba Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan iko tayari kuendelea kuimarisha uhusiano wa kimaendeleo kwa faida ya wananchi wa nchi hizo mbili na itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta hiyo ambapo ndani ya miezi mitano iliyopita kuanzia Februari, Ufaransa imeipatia Tanzania Euro milioni 330 kiasi ambacho kikubwa kwa utekelezaji miradi ya maendeleo nchini.
“Nchi zetu mbili zina urafiki ambao umekuwa ukikua kama inavyojidhihirisha katika miradi ya maendeleo tunayofadhili ikihusisha mkataba tuliosaini leo (jana). Tutaendelea kushirikiana hasa katika sekta hizi tatu ambazo ni maji na usafi wa mazingira, nishati na usafirishaji na uchukuzi,” alisema.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkazi wa AFD Tanzania, Stephanie Mouen, alisema kutiwa saini mkataba huo ni moja ya malengo ya kudumisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa.
Alisema tangu mwaka 2014 Ufaransa imewekeza zaidi ya Euro bilioni moja za utekelezaji miradi ya maendeleo duniani zikiwa jitihada za nchi hiyo kuziwezesha nchi zinazoendelea kuondokana na uhaba wa maji na uharibifu wa mazingira.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, alishukuru kutiwa saini mkataba huo kwani utasaidia wananchi wa Shinyanga ambao sasa wanapata maji kwa wastani wa asilimia 60.
Alisema kukamilika mradi huo kutafikisha maji kwa asilimia 95 au zaidi ukiwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo imeelekeza kufikia mwaka 2025 huduma ya maji mijini ifikie asilimia 95 na maji vijijini iwe asilimia 85.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa nchi yetu ya kuaminiwa na nchi mbalimbali, marafiki ambao sasa wanatukopesha kwa masharti nafuu ili kutekeleza miradi hii ya kimkakati na kuhakikisha tatizo la maji katika maeneo mbalimbali linamalizika,” alisema Mhandisi Sanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, alisema msaada huo uendelee kuwepo hadi kukamilika mradi wa maji.
“Sisi SHUWASA tuna furaha sana kupokea fedha hizi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu wa maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Shinyanga, pia miji midogo ya Tinde, Didia na Isalamagazi maalumu kwa ajili ya kuendeleza huduma za maji safi na usafi wa mazingira,” alisema Mhandisi Katopola.
Na MWANDISHI WETU