MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kiwango cha ugonjwa wa kisukari visiwani Zanzibar kimeongezeka kwa kasi kubwa.
Pia, amesema maradhi hayo kwa sasa yanawaathiri hata watoto wadogo, huku watu wenye kipato cha chini wakiwa ni waathirika zaidi wa maradhi hayo tofauti na ilivyokuwa zamani kuwa maradhi ya matajiri.
Kauli hiyo aliitoa katika Viwanja vya Mapinduzi Michenzani jijini Zanzibar, alipozungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Othman alisema mbali na Zanzibar kuwa na maambukizi ya kisukari, pia kiwango cha tatizo la maradhi ya kisukari limeongezeka sehemu mbalimbali duniani.
Alisema utamaduni wa ulaji wa vyakula na namna jamii inavyoishi uliojengeka miongoni mwa jamii imekuwa ni chachu ya chimbuko kubwa la ongezeko la maradhi ya kisukari visiwani Zanzibar.
Pia, Othman ameitaka jamii ya wananchi visiwani humo kupunguza utamaduni wa kula vyakula vyenye mafuta mengi, wanga na sukari kwa wingi ili kuepuka uwezekano wa kupata kisukari.
”Vyakula vyenye mafuta mengi ndio chimbuko kubwa la kupata maradhi ya kisukari. Jamii inapaswa kubadilika, huku ikiacha mtindo wa kuwapa watoto vyakula vyenye sukari,” alisema.
Kulingana na Othman ugonjwa wa kisukari hivi sasa umeingiwa na janga la maradhi ya Uviko-19 na hivyo kuchangia kuwepo athari kubwa zaidi kwa wagonjwa wa kisukari, ambao wanaathirika kwa wepesi zaidi pindi wakipata ugonjwa wa korona.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alisema mgonjwa mwenye kisukari anaweza kuathirika zaidi iwapo atapata ugonjwa wa Uviko-19 na hivyo kuwataka watu wote Zanzibar kuchanja kwa kuwa chanjo ziko za kutosha Zanzibar.
Alisema ni wajibu wa jamii kufahamu ipasavyo vichocheo vya maradhi ya kisukari ambayo yanashika kasi katika nchi zenye uchumi mdogo duniani ikiwemo Zanzibar.
NA EMMANUEL MOHAMED,ZANZIBAR



























