SAFARI ya saa kadhaa ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika miji na vijiji vya mikoa ya Geita na Kagera, imeacha raha tupu kwa wakazi wa maeneo hayo, baada ya ujumbe wa viongozi alioambatana nao, kueleza kwa kina, mipango ya serikali ya muda mfupi na mrefu yenye lengo la kuwagusa wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, maji na mifugo.
Baadhi ya taarifa zilizogusa mioyo ya wananchi ni kupanda kwa bei ya kahawa na pamba sokoni, mpango wa serikali kuyaunganisha na gridi ya taifa maeneo yaliyo nje ya mfumo huo, dhamira ya kutekeleza miradi mikubwa ya maji, ujenzi wa barabara, hospitali na maboresho katika ugawaji wa vitambulisho vya taifa.
Hali hiyo ilijitokeza wakati mawaziri husika wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo ambayo msafara wa Rais Samia ulipita kutokea Kiwanja cha Ndege cha Chato, kwenda mkoani Kagera, ambako atakuwa na ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia leo.
Akizungumza mbele ya Rais Samia, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema serikali ina mpango wa kuunganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa na mradi wa maji, kwa lengo la kuwasaidia wananchi kufanya kilimo cha umwagiliaji na kuepukana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Bashe alisema kuanzia mwaka ujao wa fedha, serikali itatoa ruzuku kwa ajili ya mbolea ili
kupunguza gharama iliyopo sokoni huku akisisitiza kuwa, bei ya mazao yakiwemo pamba na kahawa, itaendelea kupanda kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali.
Alisema: “Bei ya kahawa imepanda, ni zao linalofanya vizuri sana kwa sasa na mnada wa mwisho Ngara, Arabika imeuzwa kwa sh. 3,700 na Robusta bado ipo kwenye sh. 1,200 kwa kilo, lakini tunaendelea kuchapa kazi, bei hii itapanda tu.
“Kwenye pamba, nako tunafanya vizuri na niseme muda wa kuibia wakulima umepita, tunaagiza mnada wa wazi tutapeleka TV wakulima waone wazi…hawataweza kutupiga kwa sababu bei ya soko la dunia tunaijua.”
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema kwa mkoa wa Kagera pekee, miradi mikubwa 78 ya maji, inaendelea kutekelezwa, kati ya hiyo, miradi 13 inapatikana Biharamulo.
Alisema serikali itaendelea kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani kwa kuwafuatilia wakandarasi wanaokabidhiwa miradi hiyo, ili ikamilike kwa wakati na viwango kwa lengo la kuwasaidia wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa, alisema serikali ina mpango wa kutoa sh. milioni 204, ambazo awali zilirudishwa serikalini kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya Biharamulo.
Alisema barabara iliyopo katikati ya wilaya hiyo, yenye urefu wa kilomita mbili, itajengwa kwa kiwango cha lami na kufungwa taa za barabarani kama alivyoagiza Rais Samia, ili wananchi wapate fursa ya kufanya biashara hadi usiku na kujiongezea kipato.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni, alisema serikali ina taarifa kuhusu changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho vya uraia katika maeneo mbalimbali ukiwemo mkoa wa Kagera, ambako ni karibu na mpaka wa nchi jirani.
Alisema tayari Rais Samia, ametoa sh. bilioni 42.5 kwa ajili ya manunuzi ya kadi ghafi za vitambulisho, ambazo zitasaidia kwenye utengenezaji wa vitambulisho vipya ili wote wenye uhitaji na sifa za kuwa na vitambulisho hivyo wapate bila usumbufu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, alisema serikali imefanya upembuzi yakinifu na kubaini vituo 18 katika mkoa wa Kagera ambavyo vitajengewa vizimba vya kisasa vya kufugia samaki, ili kuwasaidia wavuvi kutekeleza majukumu yao.
Stephen Byabato, ambaye ni Naibu Waziri wa Nishati, alibainisha kuwa, serikali itaendelea na kasi kubwa zaidi ya kufungia wananchi umeme vijijini na mijini na kwamba kwa wilaya ya Muleba, serikali imetoa sh. bilioni sita kwa ajili ya kazi hiyo.
BODABODA WACHEKELEA
Madereva pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda mkoani Kagera, walikuwa miongoni mwa mamia ya watu waliojitokeza kumlaki Rais Samia, ambapo walitumia fursa hiyo kumpongeza kwa kupungua bei ya mafuta sokoni.
Pongezi za bodaboda hao ziliwasilishwa na Umoja wa Bodaboda Wilaya ya Bukoba (UBOBU), ikiwa siku moja kabla ya Rais Samia kufika mkoani Kagera kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.
Mwenyekiti wa UBOBU, Mahamud Sued, alisema ushushaji wa bei ya mafuta utalisaidia kundi kubwa la bodaboda kumudu gharama za maisha na kuepuka kujiingiza kwenye vitendo viovu.
“Ili kutambua ukubwa wa kundi hili kwa upande wa Manispaa ya Bukoba pekee kuna bodaboda 8,600 ndio maana tunaomba aendelee kutupunguzia gharama. Ruzuku imetolewa kwa wakati muafaka na kutupa nahueni sisi ambao riziki zetu zinategemea sana bei ya mafuta,” alisema.
Alisema kabla ya kutolewa kwa ruzuku hiyo, kwa Bukoba mafuta yalikuwa yanauzwa sh. 3,460 kwa lita na sasa yanauzwa sh. 3,200 kwa lita kukiwa na punguzo ya sh. 260 kwa lita.
“Pia bodaboda tunamuomba Rais Samia kurasimisha biashara ya bodaboda na kulitambua kama kundi maalum lenye uhitaji wa kuwekewa mazingira mazuri ya kibiashara kama inavyofanyika kwa wamachinga.
Na MWANDISHI WETU

Rais Samia ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kagera kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo ya Wananchi.