KATIKA muendelezo wa juhudi za kufungua milango ya biashara na kuvutia uwekezaji Tanznaia, Ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka sekta binafsi umeondoka nchini kwenda Marekani kwa ziara ya kibiashara.
Ziara hiyo ni matokeo ya maombi ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, kutaka kukutana na wafanyabiashara wakubwa nchini Marekani, alipokutana na Balozi anayeiwakilisha nchi hiyo Tanzania, Dk. Donald Wright.
Katika taarifa ya TPSF, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Francis Nanai, ujumbe huo unaongozwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, ukilenga kukutana na makundi mbalimbali ya wawekezaji.
Taarifa hiyo inaeleza, wawekezaji wakubwa watakaokutana na ujumbe huo ni wa sekta za afya, utalii, miundombinu, kilimo na teknolojia ya habari.
Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za TPSF kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara, kuvutia wawekezaji wa nje na ndani na kuitangaza Tanzania.
“Ziara hii ni sehemu ya jitihada za sekta binafsi za kuunga mkono juhudi kubwa za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji wa nje na ndani, pamoja na kazi kubwa anayoifanya ya ‘Re-Branding’ Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, taarifa inafafanua kuwa, ziara hiyo ni matokeo ya maombi ya Mwenyekiti wa TPSF kwa Balozi Dk. Wright, kutaka kukutana na wafanyabiashara wa Marekani ili kuwaunganisha.
“Katika mkutano huo, Mwenyekiti alimwomba Balozi kusaidia sekta binafsi ya Tanzania kuwaunganisha na wawekezaji wakubwa wa Marekani ili waungane na wafanyabiashara wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya ubia (Public Private Partnership).
Kuwekeza katika sekta za utalii, uvuvi, afya, miundombinu, ujenzi wa Industrial Parks na kukuza biashara na masoko kupitia mpango wa AGOA,” iliandika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara ya ujumbe huo imeandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na taasisi ya Marekani Corporate Council on Africa.
“Taasisi ya Sekta Binafsi inapenda kuishukuru serikali kupitia Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ubalozi wa Tanzania New York na Washington Marekani na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha ziara hii,” ilisema.