Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, ameitaka Israel kuheshimu sheria za kimataifa wakati ikifanya operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Guterres amesema amefadhaishwa na tangazo la Israel kuwa ingeweka mzingiro kamili dhidi ya ukanda huo ikizuia kikamilifu kuingizwa kwa chakula, maji na nishati ya umeme. Pia amelaani mashambulizi ya makombora ya hospitali na makazi katika Ukanda wa Gaza, akiomba UN iruhusiwe kuingia kutoa misaada ya kibinadamu.
Aidha, Guterres amelaani kitendo cha Hamas kuwateka mateka raia na wanajeshi, pia ameelezea wasiwasi wake juu ya ripoti za zaidi ya Wapalestina 500 waliouawa huko Gaza.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, amesema vita baina ya Israel na Hamas, havipaswi kuchochea zaidi moto wa uhasama na kuongeza kuwa ugaidi hautashinda.
DW