KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, amesema kuna ulazima wa watu wote duniani kupata chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Guterres ametoa msimamo huo katika ujumbe wake aliouweka katika ukurasa wa twitter kuwa njia moja ya kusonga mbele mwanadamu ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali kubwa na kusogeza mbele malengo ya maendeleo.
Aliandika ”Ni kuitaka jamii ya kimataifa kufanya juhudi ili watu wote duniani wapate chanjo ya kujikinga na corona. Mapigano, njaa, umaskini na hali ya migogoro yote hayo yanakumbusha namna kulivyo na pengo kubwa la matabaka duniani”.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, jamii ya kimataifa inapasa kulinda haki na heshima ya watu wote khususan matabaka ya watu maskini na walionyongeshwa pakubwa wakiwemo wanawake na mabinti, watoto na vijana.
Tamko hilo la Katibu Mkuu wa UN limekuja wakati ambao taasisi na mashirika ya kimataifa yamekuwa yakilalamikia mgawanyo usiokuwa bora wa chanjo za corona duniani.
Kuhusiana na suala hilo, viongozi wa ngazi ya juu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wamezitaka nchi tajiri duniani ikiwemo Marekani badala ya kuanza kutoa dozi ya tatu ya corona zitoe chanjo hizo kwa mpango wa kimataifa wa COVAX.
Lengo la kuzitoa chanjo hizo ili ziwezwe kutumwa katika nchi mbalimbali duniani zenye kipato cha chini. DW