WAANDISHI WETU, MIKOANI
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Raymond Mwangwala, amewatoa hofu vijana kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli na kuwahakikishia nchi imejengwa kwa misingi imara.
Mwangala, aliyasema hayo jana, ofisini kwake Dodoma, wakati akizungumza na gazeti hili, akiwasihi vijana kuyaishi mema yaliyofanywa na Rais Dk. Magufuli enzi za uhai wake, akiwa madarakani.
Katika uongozi wake, aliteua vijana kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Ni kiongozi ambaye aliangalia uwezo wa mtu, tumepoteza jemedari wa Afrika. Tutaenzi falsafa zake alizoanza kuzijenga kwa vijana, amefariki katika kipindi ambacho hatuajwahi kupata kiongozi mkubwa kufariki akiwa madarakani,” alieleza.
Pia, alieleza msiba huo umeacha fundisho kwa Watanzania kujituma kwa kufanya kazi, kumpenda Mungu na kufuata ujasiri aliokuwa nao Rais Dk. Magufuli.
Cha msingi cha kuwaambia vijana na wananchi ni kwamba, nchi itaendelea kuwa salama, tunaamini wapo viongozi wenye uwezo mkubwa waliojengwa katika uzalendo na upendo kwa taifa, tuendelee kuliombea Mungu atupatie nguvu ya kuhimili hili,alibainisha.
WANANCHI WANENA
Nao, baadhi ya wananchi mkoani hapa, walieleza namna walivyoguswa na msiba wa Rais Dk. Magufuli, ambapo mfanyabishara wa Soko la Majengo, Abdalah Omary, alisema hakutarajia kupokea taarifa za msiba huo kwa wakati huu, kwa sababu alikuwa analipeleka taifa mahali ambapo Watanzania walikuwa wanatamani kufika.
“Nimeumia sana, natamani kama ningekuwa na uwezo ningemrudisha Rais wangu angalau atuage Watanzania, kwa sababu aliyoyafanya ni ishara tosha ya upendo wake kwetu,” alisema.
Muuza samaki kwenye soko la Bonanza, Right William, alisema imekuwa ghafla kumpoteza kiongozi jasiri na mbeba maono ya Watanzania, hasa wananchi wanyonge.
“Sina cha kusema, huyu baba (Magufuli), Mungu amlaze mahali pema peponi kwa sababu hata watoto wadogo wanajua mchango wake kwao, kitendo cha kufanya elimu bure, hii ni nembo ambayo ameacha na hatokuja kusahaulika kamwe,” alieleza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nduka, Kata ya Chamwino, Mohamed Pampai, aliwataka Watanzania kuwa na umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu ambacho kila Mtanzania ana majonzi.
MAGUFULI NA USAWA
Baadhi ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera, wamepokea kwa huzuni taarifa za kifo cha Rais Dk. Magufuli huku mkazi wa Manispaa ya Bukoba, Christina Mnoku, akisema Rais Dk. Magufuli alipenda kujenga taifa na jamii yenye usawa kwa watu wote bila kulinganisha hali zao na vipato vyao.
Mzee Magufuli, hakuona shida kuchukiwa na wachache ili kufanya mambo ambayo yananufaisha taifa, kwake aliamini kiongozi ni kuwanufaisha walio chini yake na kuwatumikia wanachi kwa kuwaondolea kero ambazo zinawaumiza,” alisema.
Naye, Alistides Mwinuka, alisema vijana hawakuaminiwa wakati uliopita, lakini Rais Dk. Magufuli, alionyesha kuwaamini na kuwapa nafasi kubwa katika uongozi, ambapo awali viongozi wengi walitilia mashaka kuwapa nafasi za ngazi za juu vijana.
WAJASIRIAMALI WAJAWA MASIKITIKO
Wananchi wa Mkoa wa Arusha na viunga vyake, wamepokea kwa masikitiko kifo cha Rais Dk. Magufuli, kilichotekea jana, katika Hospitali ya Mzena, iliyoko Jijini Dar es Salaam.
Neema John, mkazi wa Mkoa wa Arusha, alisema kwa kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Magufuli, wanawake walipata faraja kubwa ya kupata mikopo, ambayo imewakwamua kiuchumi.
“Ni pigo kubwa kwa taifa, tunasikitika sana kuondokewa na Rais wetu kipenzi cha wengi, tulimpenda kwa sababu alitupenda na kututhamini sana wanawake,” alieleza.
Alisema Rais Dk. Magufuli, amewatua ndoo kichwani wanawake wa Mkoa wa Arusha, kwa kuleta mradi mkubwa wa sh. bilioni 520, na baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Arumeru.
“Licha ya Jiji la Arusha na Wilaya ya Arumeru, pia alifanikisha ujenzi mkubwa wa mradi wa maji wa shilingi bilioni 15.8, kutoka Mto Simba, uliopo Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro hadi Longido, ambayo tangu Uhuru, haikuwahi kupata maji ya bomba kama hivi sasa, ambavyo wananchi hao wanatumia maji hayo kwa mtumizi ya nyumbani na mifugo,” alieleza.
Musa Diva, ambaye ni wakala wa mabasi stendi kuu ya mabasi mkoani Arusha, alisema amesikitishwa na kifo cha Rais Dk. Magufuli, baada ya kupata tarifa hizo.
Amina Njoka, machinga katika Mtaa wa Kariakoo, Jijini Arusha, alisema ni pigo kubwa kwa machinga katika Mkoa wa Arusha kwa sababu walikuwa wanafanya biashara zao kwenye eneo lolote.