UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Dar es Salaam, unatarajia kutoa mafunzo kwa wanawake 200 wenye ulemavu, jinsi ya kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini.
Pia, inatarajia kutoa semina kwa wajane 200, mafunzo ambayo yanalenga elimu ya kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchuimi.
Akizungumza na UhuruOnline, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, Florence Masunga, amesema semina kwa watu wenye ulemavu inatarajiwa kufanyika Septemba 23 na 24, mwaka huu, ikiwa ni mfululizo wa jitihada za umoja huo za kuwafungulia fursa wanawake ili wanufaike nazo.
Amesema semina hizo zitashirikisha wawezeshaji kutoka sekta zote muhimu, zikiwemo za viwanda, kilimo, biashara, siasa, elimu na fedha.
Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa dhamira yao ni kutaka wanawake kushika uchumi na nyanja za uamuzi na kufikia malengo ya asilimia 50 kwa 50 ya wanawake na wanaume katika nyanja hiyo.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, ametuonyesha njia sisi wanawake na sasa tushindwe wenyewe,” amesema Florence Masunga.
Amewataka wanawake kupendana na kuufuta usemi wa adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe.
“UWT Dar es Salaam ni moto na watakaoshiriki semina wataambiwa watakachoenda kufanya. Hawatapoteza muda wao wa kukaa katika semina bure,” amesisitiza.
Florence amesema semina hizo zimepata ufadhili kutoka kwa taasisi binafsi ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TASWE-Saccos) inayoongozwa na mjasiriamali Ane Matinde.
Aidha, amesema wanataka ikifika mwishoni mwa Novemba, mwaka huu, UWT Dar es Salaam iwe imetekeleza maagizo yaliyotolewa na viongozi wao wa ngazi za juu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za makatibu wa UWT kwa wilaya zote sita na vitega uchumi.
Na CHRISTOPHER LISSA