MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Lindi, Aisha Issa, amezindua Wiki ya Umoja huo kwa kuwatembelea wafungwa wanawake katika magereza na kufanya usafi katika kituo cha afya Mnazi Mmoja, Manispaa ya Lindi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Aisha amesema kutokana na kaulimbiu ya wiki hiyo isemayo: ‘tushiriki kumkomboa mwanamke kiuchumi, kifikra na kisiasa’ wameamua kutoa sadaka kwa wanawake magerezani na hospitalini.
Aisha amesema wameona maadhimisho hayo ni chachu ya kuwatembelea wanawake wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali na kutoa sadaka, ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwafikia wanawake ambao wanahitaji msaada.
“Ni jukumu la kila mwanamke kuhakikisha tunawafikia wanawake wenzetu kila sehemu, ili kuwapa msaada na elimu kuhusu wajibu wa mwanamke katika kazi na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kipenzi cha Watanzania,” alisema.
Aliwaomba wanawake kuunga mkono jitihada za Samia ambaye anafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM katika kila eneo nchini.
“Wanawake Mkoa wa Lindi tupo tayari kwenda na mama mpaka 2020/2025 kwa maslahi ya taifa letu kwa kufanya kazi na kutekeleza miradi,” alisema Aisha.
Katibu wa UWT Mkoa wa Lindi, Somoe Mkundapai, alisema wanawake wa Lindi wameamua kutoa sadaka hiyo kwa wenzao ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia.
“Sabuni, taulo za kike, vyakula na mahitaji mengine, tumevitoa msaada kwa wanawake wenzetu na jamii kwa ujumla, hili kwetu ni jambo endelevu na tunataka kumhakikishia Rais Samia kuwa tupo pamoja na yeye katika kuwahimiza wanawake wenzetu kufanya kazi kwa juhudi,” alisema Somoe.
Mkaguzi Msaidizi wa Magereza Manispaa ya Lindi, Asha Mwinyipingu, aliwapongeza wanawake wa Lindi kwa kutoa vyakula, sabuni na taulo za kike kwa wanawake walioko gerezani.
Na SOPHIA NYALUSI, Lindi