KATIBU wa Umoja wa Wanawake (UWT), Wilaya ya Temeke, Huba Issa, amesema wanaendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya kutangaza utalii nchini kupitia filamu ya Royal Tour.
Amesema, pia wanaendelea kumuombea afya njema Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu ya kuongoza nchi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Huba alisema Rais Samia anafanya kazi kubwa ya kukuza uchumi wa nchi, hivyo vizuri makundi yote yamuunge mkono kwa nguvu zote.
“Rais Samia ni kiongozi mwenye msimamo asiyeyumba, mchapa kazi mwenye ujasiri mkubwa na uhodari imara katika uongozi, hivyo tuna uhakika ataifikisha nchi yetu katika mafanikio makubwa ya kiuchumi,” alisema.
Katika kutangaza nchi kupitia filamu ya Royal Tour, Katibu huyo wa UWT alisema Rais Samia ameweka rekodi kubwa nchini itakayoinua uchumi.
Alisema wanawake wa Temeke wapo bega kwa bega na Rais Samia katika kutangaza utalii na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Kuhusu sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu, katibu huyo alisema wanaendelea kuhamasisha wananchi kwa ajili ya kuhakikisha wakati utakapowadia wanatoa ushirikiano kwa makarani.
Na SUPERIUS ERNEST



























