VIJANA nchini wameaswa kuenzi na kuishi fikra za waasisi wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ili wawe wazalendo na kudumisha tunu za taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa Mdahalo wa Vijana Kitaifa uliofanyika katika Shule Sekondari Chato mkoani Geita.
Waziri Jenista alieleza kuwa kuna sababu za msingi za kuwakumbuka waasisi wa taifa, ambao ni Baba wa Taifa na Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Karume, kwa mchango wao mkubwa usiosahaulika kwa Taifa.
“Mchango huu wa waasisi wetu ni vyema urithishwe kwa vizazi vilivyopo hususan vijana na vizazi vijavyo ili waweze kuwa wazalendo kwa taifa lao na wakaziishi falsafa za viongozi hao,” alieleza Waziri Jenista.
Alisema vijana wanapaswa kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake na Mzee Karume ili waendelee kujivunia juu ya misingi ya amani na umoja iliyopo nchini.
Aidha alifafanua kuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kujenga umoja wa Kitaifa na kudumisha amani.
“Baba wa Taifa, aliasisi Mwenge wa Uhuru mwaka 1961 mara tu nchi yetu ilipopata Uhuru, lengo lilikuwa ni kuutumia Mwenge wa Uhuru kama chombo cha kuhamasisha ujenzi wa Taifa lenye watu wenye amani, lenye watu wenye upendo, lenye watu wenye matumaini na lenye watu wenye heshima,” alisema.
Pamoja na hayo alisisitiza vijana na wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuendeleza maono ya waasisi wa taifa na kuleta mageuzi ya kiuchumi yenye manufaa kwa taifa.
Waziri Jenista alitumia fursa hiyo, kuwahimiza wananchi na wakazi wa Chato kushiriki kwenye Maonesho ya Wiki ya Vijana, ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Mazaina, sambamba na kushiriki kwenye kilele cha Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika Uwanja wa Magufuli Chato mkoani Geita Oktoba 14 mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, alisema ni vyema vijana wakatumia fursa ya mdahao huo ili waweze kutambua vyema historia ya Waasisi wa Taifa na kutambua maudhui ya Mwenge wa uhuru ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha Watanzania na kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii ili wajiletee maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Richard Jaba, akitoa salamu wakati wa mdahalo huo, alisema ni heshima kubwa kwa vijana kupata fursa za kujumuika pamoja na kueleza masuala yao.
Alipongeza uamuzi wa shughuli hizo kufanyika katika mkoa wa Geita na kuwaasa vijana kuendeleza umoja, mshikamano na upendo ili kuendelea kuchangia katika kuleta maendeleo nchini.
“Kalenda ya Chama inatambua uwepo wa wiki la vijana, hivyo tunaunga mkono kwa vitendo uwepo wa mdahalo huu na tutaendelea kutoa ushirikiano kwenu pia tunashukuru kuleta shughuli hizi Geita,”alisema Jaba.
Na Mwandishi Wetu, Chato



























