VIKUNDI 112 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu wilayani Misungwi mkoani Mwanza vilivyopewa mikopo ya sh. bilioni nne vimetakiwa kuripoti Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uhakiki.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, aliyasema hayo wakati wa mkutano na wajumbe wa kamati ya fedha, watendaji wa kata na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Amesema vikundi 112 wilayani hapo vilikopeshwa zaidi ya sh. bilioni nne na hadi sasa zimerejeshwa sh. milioni 57.
Mhandisi Gabriel alisema Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imekuwa na tabia ya kutoa mikopo kwa vikundi hewa ambavyo havina usajili, hivyo kuisaibabishia hasara serikali.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo, katika wilaya hiyo kuna vikundi hewa 17 vilivyokopeshwa zaidi ya sh. milioni 73 na havijarejesha na hutoa wiki moja kuhakikisha vinahakikiwa Takukuru.
Aidha, alitoa saa 24 kwa watumishi wa umma walionufaika na mikopo hiyo kurejesha na kuitaka Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuepuka tabia ya kuanzisha vikundi hewa.
Naye, Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Mwanza, Stella Bukulu, alisema utafiti uliofanywa na taasisi hiyo ulibaini vikundi vingi vilikopa fedha kisha wakagawana, ambapo kila mwanakikundi anafanya shughuli zake tofauti na andiko la mradi waliloombea.
Alisema katika utafiti huo waligundua tatizo la fedha za mikopo hiyo linatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kutokurejeshwa kwa wakati unaotakiwa au kutorejeshwa kabisa.
Bukulu aliweka bayana vikundi vingi ni vya kitapeli kwa kuwa baadhi vina maslahi ya kisiasa kuliko uhalisia na havilengi kuwakomboa wananchi na umasikini wa kipato.
Alisema serikali inapoteza fedha kupitia mikopo hiyo kutokana udhaifu wa mifumo ya uundaji wa vikundi, utoaji wa fedha na urejeshaji na ukosefu wa vitendea kazi unakwamisha ufuatiliaji.
Bukulu alieleza taasisi hiyo imekuwa ikifuatilia matumizi ya miradi ya serikali, ukiwemo uchambuzi wa mifumo kuangalia utendaji, sera, sheria, kanuni na taratibu.
Alisema katika ufuatiliaji huo walipata changamoto ya ushirikiano mdogo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa watendaji kushindwa kutoa nyaraka muhimu za mikataba ya kazi, matangazo ya zabuni na nyaraka za benki.
Diwani wa Kata wa Fella (CCM) Paul Kishinda, aliiomba halmashauri kutoa elimu ya utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa wananchi wake ili kuondokana na kadhia ya kutorejesha fedha hizo za umma.
NA BALTAZAR MASHAKA, Misungwi



























