POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi sugu, wanaodaiwa kujihusisha na makosa ya unyanganyi wa kutumia silaha na imekamata silaha aina ya AK47 ikiwa na risasi 14.
Limesema watuhumiwa hao ambao ni vinara kwa makosa ya ujambazi wamekamatwa ikiwa ni mwendelezo wa operesheni kali ya kudhibiti vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ndani ya kanda hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Muliro Jumanne, alisema watuhumiwa hao ni vinara wa matukio ya unyanganyi,wizi wa magari na pikipiki ambapo walikamatwa wakiwa na pikipiki 11 na Televisheni 23.
“Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata majambazi sugu, majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za upelelezi ambao ni vinara wa matukio ya unyanganyi wa kutumia silaha, uvunjaji, wizi wa magari ,pikipiki .
“Wahalifu hawa walikamatwa na kukutwa na baadhi ya vifaa vya magari yaliyoibwa ,vifaa vya pikipiki 11 za wizi na televisheni 23,” amesema
Kamanda Muliro amesema silaha ya AK47 ilikamatwa Oktoba 22, saa 3.00 usiku, eneo la Tegeta, baada ya jambazi mmoja kutaka kupora ambao walikuwa wakirushiana risasi na askali wa polisi ambaye baadaye alikimbia na kuiacha silaha hiyo.
“Kabla ya kutekeleza adhima yake alikurupushwa na kikosi kazi cha kuzuia na kupambana na ujambazi,ambapo walirushiana risasi kwa muda kadhaa na hatimaye jamabazi huyo aliitupa bunduki hiyo na kukimbia ,hata hivyo msako mkali dhidi ya wahusika na wenzake unaendelea na lazima watakamtwa,” amesema.
Amesema wanamshikilia mtuhumiwa Shukuru Nassoro na wengine 20 kwa kujihusisha na matukio ya ukwapuaji kwa kutumia pikipiki pamoja na wizi wa vifaa vya magari na kununua vifaa hivyo.
Kamanda Muliro amesema wamebaini watuhumiwa hao wamekuwa katika mzunguko wa kisheria kwenye Taasisi za Polisi, Mahakama na Magereza.
Pia, Kamanda Muliro amesema wanawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mbezi Msumi katika Wilaya ya Ubungo tukio lilotokea Oktoba 11, mwaka huu, ambapo marehemu alikatwakatwa mapanga akiwa ofisini kwake.
Aidha, Kamada Muliro amesema Kikosi Kazi cha Jeshi la Polisi kimemkamata Ramadhani Francis,(24), aliyekuwa akitumia bastola bandia kufanyia uhalifu.
“Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata majambazi sugu, majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za upelelezi ambao ni vinara wa matukio ya unyanganyi wa kutumia silaha, uvunjaji, wizi wa magari pikipiki.” Jumanne Muliro
Na IRENE MWASOMOLA