MABONDIA 24 wanatarajia kupanda ulingoni katika pambano la ‘Usiku wa Nyodo’ utakaofanyika Julai 17, mwaka huu, katika Uwanja wa Kinesi uliopo Urafiki, Dar es Salaam.
Akizungumzia usiku huo, Muandaji wa pambano hilo, Selemani Semunyu, amesema maandalizi yamekamilika, mabondia wamejipanga vizuri ili kutoa burudani kali.
Semunyu ameeleza kuwa, pambano kubwa litakuwa kati ya Ibrahim Tamba dhidi ya Hussein Itamba, ambao watacheza mzunguko wa raundi 10 uzani wa kilo 76.
“Maandalizi yamekamilika, pambano hilo kuelekea katika pambano la marudiano kati ya Twaha Kassimu ‘Twaha Kiduku’ na Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe litakalofanyika Agosti 20, mwaka huu, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam,” amesema Semunyu.
Muandaaji huyo ametaja baadhi ya mabondia watakaozichapa katika pambano hilo kuwa ni Paul Magesta, atakayezichapa na Hassan Ndonga; Ally Gonywa dhidi ya Omari Mpemba; Abdallah Ubaya atapigana na Pius Mpenda; Dorethea Muhoza atamenyama na Jesca Mfinanga na Antony Peter dhidi ya Shafii Vikiru.
Na Amina Kasheba