MKURUGENZI wa kampuni ya Shangri La Investiment, Xiukun Chen na mwenzake wamehukumiwa kulipa faini ya sh. milioni 21 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka manne, likiwemo la kuajiri raia wa kigeni bila ya kuwa na kibali.
Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Yunlong Gu, raia wa China, ambaye alikuwa mtafiti wa kampuni hiyo. Washitakiwa hao walilipa faini.
Washitakiwa hao walipewa adhabu hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya kukiri mashitaka yanayowakabili.
Mashitaka hayo ni kufanya kazi bila kuwa na kibali cha makazi na kazi, kumwajiri raia wa kigeni bila kuwa na kibali cha makazi na kibali cha kazi.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao walitenda makosa hayo Agosti 18, mwaka huu, eneo la Sandali, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, katika kampuni ya Shangri La Investiment.
Akitoa adhabu hiyo, Hakimu alisema shtaka la kwanza na la nne kila mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya sh. 500,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Katika shtaka la pili na la tatu, kila mshitaka atatakiwa kulipa faini ya sh. milioni 10 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Pia, Mahakama imeamuru mshitakiwa wa pili kurudishwa nchini kwao baada ya kumaliza adhabu. Washitakiwa hao walifanikiwa kulipa faini hiyo.
Awali, Wakili wa Serikali, Shija Sita, aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine huku washitakiwa hao, wakiomba wasipewe adhabu kali kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza.
Na REHEMA MOHAMED



























