SIKU chache baada ya uongozi wa klabu ya Simba kumtangaza Kocha mpya, Pablo Franco, kuchukua mikoba ya Mfaransa, Didier Gomes, aliyefukuzwa mwishoni mwa mwezi uliopita, wadau wa soka nchini wamefunguka kuhusu ujio wake.
Franco ambaye ni raia wa Hispania, ni kocha mwenye uzoefu aliyefundisha klabu mbalimbali nchini kwao, ikiwemo mabingwa wa kihistoria wa Hispania, Real Madrid.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mchambuzi wa soka nchini Ali Mayai alisema ukiangalia wasifu wa kocha huyo, hajawahi kufundisha soka Afrika hii ni mara yake ya kwanza, hivyo anatakiwa kutumia muda mwingi kwa ajili ya kujifunza na kuisoma timu yake na michuano inayoshiriki kwa ujumla.
Alisema kwa sasa hawezi kuwa na kitu kipya hadi akisome kikosi chake kwa muda mrefu, baada ya hapo ndio aje na programu zake mpya.
“Ukiangalia wasifu wake na timu alizozifundisha ni kocha mzuri, lakini anatakiwa awe na muda mrefu wa kukisoma kikosi chake ndio aanze programu mpya, hii itamsaidia sana sababu ni kocha ambaye bado hajajua soka la Afrika,” alisema Mayai.
Mchambuzi na kocha Joseph Kanakamfumu, alisema ni kocha mzuri kuja nchini, hivyo uzoefu wake utambeba kwa kiasi kikubwa kwani ameshapita katika timu mbalimbali zenye ubora zaidi ya Simba.
Aliongeza kuwa, kutokana na uzoefu wake katika soka, anaweza kuisaidia Simba ikaendelea kuweka rekodi nzuri za kutwaa mataji msimu huu.
Alisema ni mapema sana kuanza kumzungumzia, lakini wanasubiria kuona kazi yake atakapokuwa ameisimamia timu, lakini wasifu wake unaridhisha kwa kiasi kikubwa.
“Mashabiki kwa sasa wanatakiwa kuwa wavumilivu na kumpa muda kwani ni kocha ambaye hajawahi kufundisha soka la Afrika, hivyo wanatakiwa wawe na imani naye ili kuhakikisha wanampa ushirikiano wakutosha.
“Kwanza lazima azitambue falsafa za timu za Tanzania na ligi kwa ujumla, ndio aje na mipango yake, anatakiwa kupewa muda wakutosha ili kuifanya timu iendeleze rekodi zake za kutwaa mataji msimu huu,” alisema Kanakamfumu.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenedy Mwaisabula, alisema hana mashaka na kocha huyo kikubwa anatakiwa apewe muda na aachiwe timu ili aweze kuitengeneza na asiingiliwe katika majukumu yake.
“Ni kocha mzuri ambaye naona ataenda kuisaidia Simba, kikubwa anatakiwa apewe muda mwingi kwa ajili ya kuijenga timu na wasiwe na haraka kwani kocha hawezi kuitengeneza timu kwa muda mfupi,” alisema Mwaisabula.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 41, mzaliwa wa Madrid, Hispania, alianza kufundisha timu ya Coria mwaka 2008 hadi 2009 akaenda Fuenlabrada timu zote akiwa kocha msaidizi.
Mwaka 2010 alikuwa Kocha Mkuu wa Santa Eugenia hadi 2012, akahamia Puertollano hadi 2014, akaenda Getafe B hadi 2015 Getafe A katika Ligi Kuu ya Hispania hadi 2016, akahamia Saburtalo Tbilisi ya Georgia hadi 2017.
Baada ya hapo, akatua BSU ya China hadi aliporejea Hispania na kuwa Kocha Msaidizi wa Real Madrid hadi 2019 alipojiunga na Al-Qadsia ya Kuwait hadi alipokubali kujiunga na Simba mwezi huu.
Na NASRA KITANA