WAHITIMU wa mafunzo ya muda mfupi katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), wamehimizwa kuhakikisha wanatumia elimu waliyoipata kuwanufaisha na kuifanya ajira ya kujiingizia kipato.
Hayo yamesemwa na Ofisa Elimu wa Sekondari Bagamoyo, Alois Kaziyareli, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Zainab Abdallah, wakati wa mahafali ya wanafunzi hao waliohitimu mafunzo ya mwezi mmoja.
“Wahitimu wote tunawaasa mkatumie vyema mafunzo mliyoyapata ili kuhakikisha mnanufaika nayo na kuwa ajira ambayo itawasaidia kuingiza kipato,” alisema.
Mkuu wa TaSUBa, Herbet Makoye, amesema wanajivunia kufanya kazi na taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa zikipeleka wanafunzi chuoni hapo, hivyo wakawe mabalozi wazuri kwa kuwashawishi wengine kujiunga na mafunzo.
“Tunajivunia kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa zikileta wanafunzi wao chuoni hapa, tunatarajia mtakwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kuwashawishi wengine ili waje kujiunga na masomo katika muhula mpya,” amesema Dk. Makoye.
Mhitimu kutoka Kanisa la Waadventista wa Sabato, Rebbeca Byeye, amesema anatarajia kutumia mafunzo aliyoyapata ili kuhakikisha anaendeleza kipaji chake.
Amesema awali wakati anaingia chuoni kuna mambo ambayo alikuwa hayaelewi, lakini elimu aliyoipata imempa mwanga kwa kiasi kikubwa.
Na MWANDISHI WETU, Bagamoyo