WAKATI michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikielekea ukingoni, vita ya ufungaji bora msimu huu imezidi kushika hatamu, washambuliaji wanapambana bila kuchoka.
Katika vita hiyo, straika George Mpole anayekipiga Geita Gold na Fiston Mayele wa Yanga wamekuwa wkichuana kwa karibu, wachezaji hao wameonyesha vita ambayo kila mmoja anataka kushinda.
Hadi sasa, michuano hiyo imechezwa kwa raundi 29, imebaki raundi moja kabla ya ligi kumalizika.
Ukiwa umsalia mchezo mmoja kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo, vita kubwa ya ufungaji bora imebaki kwa Mayele na Mpole ambao wakipania kiatu cha ufungaji bora msimu huu.
GEORGE MPOLE (MABAO 16)
Straika huyo mzawa anayekipiga Geita Gold, kabla ya mchezo wa wikiendi hii alikuwa amefunga mabao 16 sawa na Mayele.
Mpole mwenye uchu wa mabao, amezifunga Mbeya City, Kagera Sugar, Ruvu Shooting, Polisi Tanzania, Coastal Union, Namungo, KMC, Azam FC, Mbeya Kwanza, Simba, Dodoma Jiji na Biashara United.
Katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Mpole alipachika mabao matatu, mabao mawili dhidi ya Mbeya Kwanza na Mbeya City wakati amefunga bao moja dhidi ya timu za Ruvu Shooting, Polisi, Coastal Union, Namungo, KMC, Azam FC, Simba, Dodoma Jiji na Biashara United.
Pamoja na kufunga, mshambuliaji huyo ametoa pasi tatu zilizozaa mabao.
FISTON MAYELE (MABAO 16)
Moja kati ya sababu ya Yanga kutwaa ubingwa msimu huu ni ubora wa straika Fiston Mayele.
Mabao ya mchezaji huyo yamekuwa na mchango mkubwa wa kikosi cha kocha Nasreddine Nabi kutwaa ubingwa wa ligi na kufuta mwiko wa kutotwaa kwa misimu minne mfululizo.
Mayele amefunga mabao 16 kati ya mabao 47 iliyofunga Yanga katika michezo 28 ya Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya mchezo wa juzi.
Mshambuliaji huyo amezifunga KMC, Azam FC, Mbeya Kwanza, Biashara United, Dodoma Jiji, Coastal Union, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Geita Gold na Namungo.
Mabao matatu amefunga katika mchezo dhidi ya Coastal Union, mawili dhidi ya Azam FC, Mbeya Kwanza, Kagera na Biashara United huku akifunga bao moja kikosi chake kilipopambana na KMC, Azam FC, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Geita Gold na Namungo.
Staa huyo ametoa pasi nne za kumalizia mabao yaliyopachikwa na wenzake.
RELIANTS LUSAJO (Mabao 10)
Ni muda mrefu tangu mchezaji Reliants Lusajo ashindwe kuuendeleza moto wake wa mabao katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Straika huyo wa Namungo aliyeanza msimu kwa kasi ya kupachika mabao, hadi sasa amesalia na mabao 10 pekee.
Lusajo amefunga mabao mawili dhidi ya Coastal Union na Mtibwa Sugar wakati akifunga bao moja dhidi ya timu za Geita Gold, Kagera Sugar, Mbeya Kwanza, Biashara, Ruvu Shooting na Mbeya City.
MATHEO ANTHONY (Mabao 9)
Miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na msimu mzuri msimu huu ni Matheo Anthony, aliyepachika mabao tisa.
Mchezaji huyo wa KMC amekuwa na kiwango bora ambacho kimekuwa sababu ya kuongeza ubora wa timu yake msimu huu.
RODGERS KOLA (9)
Ingawa Azam FC haikuwa na msimu mzuri, lakini Mzambia Rodgers Kola amekuwa na ubora mkubwa na kujaribu kukisaidia kikosi chake.
Mzambia huyo mwenye umri wa miaka 32, anayecheza nafasi ya ushambuliaji wa kati na winga, amepachika mabao tisa katika kikosi hicho.
Kola alitua Azam FC mwaka jana akitokea Zanaco FC ya nchini Zambia, aliyoanza kuitumikia kuanzia mwaka 2019.
KIBU DENNIS (8)
Pengine inaweza kukushangaza, lakini Kibu Dennis ni moja kati ya washambuliaji waliopo katika orodha ya kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na Simba mwaka jana akitokea Mbeya City, amekuwa na mfululizo wa kiwango bora katika michezo ya mwisho ya kumalizia ligi.
Wakati Simba ikiwa katika nafasi ya pili, kabla ya mchezo wa jana, Kibu alifunga mabao manane na kuwa mmoja kati ya washambuliaji waliofunga mabao mengi msimu huu.
Na ABDUL DUNIA